Na Mwandishi Wetu
MAGU – MWANZA: MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Mwalim, ameahidi kuwa iwapo wataingia madarakani, serikali yake itavunja bodi zote za mazao zilizopo na kuanzisha mamlaka moja itakayoshughulikia mazao ya kimkakati nchini.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Wilayani Magu, Mwalim amesema mamlaka hiyo mpya itakuwa na jukumu la kuwalinda wakulima na kuinua thamani ya mazao yao, hususan zao la pamba.

Amebainisha kuwa pamoja na mamlaka hiyo, serikali yake itaanzisha mfuko wa fidia kwa ajili ya wakulima wa pamba ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakumba.
“Leo hii mazao ya biashara yana bodi, lakini zinafanya nini? Wanalipana mishahara na posho, lakini hazimnufaishi mkulima,” amesema Mwalim na kuongeza Serikali inapaswa kuwahudumia wakulima kupitia mamlaka yake ili heshima irudi.
Ameahidi kusimamia ujenzi wa kiwanda cha kuchambua pamba mkoani Mwanza ili kuongeza thamani ya zao hilo na kuinua kipato cha wakulima.
Akimkumbuka Mzee Paul Bomani, Mwalim amesema: “Mzee Bomani aliifanya Mwanza iwe na neema ya zao la pamba na alilinda thamani yake kwa uhodari.”
Mwalim aliwataka wananchi wa Magu kumchagua na chama chake Oktoba 29 mwaka huu, 2025.
Amesisitiza kuwa wakati umefika kwa wananchi kuwa na chama kinachotetea maslahi ya wakulima. “Utajiri wenu ni kero kwao kwa sababu Mungu aliwapa pamba iwainue. Je, leo mtaelekea wapi?” amehoji.