Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM: CHAMA cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) kimesema kitaanzisha mjadala wa elimu ndani ya siku 100 kwa lengo la kubomoa mfumo uliopo.
Akizungumza na wananchi wa Kinondoni, mgombea urais wa CHAUMMA, Salum Mwalim, amesema mabadiliko hayo yanalenga kukifanya Kiingereza kuwa nyezo muhimu ya kuwaondoa watoto katika umaskini.
“Vijana wengi wanamaliza shule lakini bado wanaishi katika nyumba za wazazi wao… ndiyo hao waliosoma katika mazingira ya shule za kawaida,” amesema.

Ameongeza kuwa tatizo la ajira ni kama bomu linalosubiri kulipuka, na si tofauti za kisiasa au kidini kama inavyodhaniwa.
“Elimu tuliyonayo leo tunatakiwa kuibomoa ili watoto wetu wanapomaliza shule wawe na ujuzi wa maisha,” amesema.

Kwa upande wake, mgombea mwenza wa urais kwa tiketi ya CHAUMMA, Devotha Minja, amesema: “CCM ilisubiri mwendokasi zipigwe mawe ndipo walete mpya? CCM inatakiwa kupumzishwa kwani imeshindwa kuwasaidia Watanzania.”