Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: “TULIKUTANA na mama ambaye alikuwa amefukuzwa kazi na alikuwa ameshakaa hospitali miezi mitano kutokana na kujifungua mtoto kabla ya siku kutimia aliyekuwa na gramu 490,”.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Doris Mollel ameeleza hayo siku chache baada ya bunge kuridhia hoja ya kuongeza muda wa likizo ya uzazi kwa mwajiriwa ambaye atajifungua mtoto njiti kwa kujumuisha na muda uliobaki kufikia wiki 40 za ujauzito huku baba akipewa siku saba za mapumziko.
Amesema Safari ya kupigia kelele hoja hiyo ilianza baada ya kwenda katika hospitali moja kwa ajili ya kukabidhi vifaa tiba na kukutana na mama huyo.

“Wakati nazungumza na mama huyo, akapita Daktari mmoja ambaye sasa hivi ni marehemu, akasema changamoto hii ni kubwa sana, wamama wengi sana hapa huwa wanafukuzwa kazi au wanachukua likizo bila malipo,
“Na bado gharama za kumlea mtoto kichwa kinauma,” amesema.
Amesema hilo ndilo lililowasukuma kuanza harakati za kutetea wanawake wanaojifungua watoto njiti kwa kushirikiana na mitandao mbalimbali ya kijami, Umoja wa Wake wa Viongozi nchini, Vyama vya siasa pamoja na Kamati za Bunge.
Amesema wakaona kuna haja ya Kushirikisha Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE), pamoja na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), hivyo kuanzia hapo sauti ikawa kubwa zaidi.

“Nafurahi sana TUCTA kwa sababu walibeba hili wazo na wakalizungumza Mei Mosi mwaka jana, Natumai Mei Mosi ya mwaka huu 2025 tutakuwa tunacheka zaidi,” amesema.
Amesema jambo hilo limeweka historia kwa Tanzania, pia Bunge limeacha alama kwa nchi.
Mdau wa Mtandao Afya ya Uzazi, Agnes Mtui amesema pamoja na sheria hiyo kupitishwa, kuna wajibu wa kufuatilia kanuni kama zimetengenezwa.
Majadiliano kuhusu hoja hiyo yalianza rasmi na wadau hao mwaka 2017 kisha kupelekwa Bungeni mwaka 2018.
Naye Makamu Mwenyekiti wa TUGHE, Dkt. Jane Madete amesema
Taasisi ya Doris Mollel inatambua umuhimu wa kuongeza siku za likizo kwa wazazi wanaopata Watoto njiti kwani kutalinda ustawi wa afya za Watoto wanaozaliwa kabla ya wakati ambao wanahitaji muda wa kutosha wa Uangalizi.