Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ameuagiza uongozi wa Wafanyabiashara Ndogo Ndogo kuanza kufungua barabara zinazoingia sokoni Kariakoo ili magari yaweze kupita.
Chalamila ametoa agizo hilo leo jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu ufunguaji wa soko hilo.

“Leo utakapokwenda soko hilo njia zake karibu zote zimefungwa na zimefungwa na wafanyabiashara ndogo ndogo ambao wameweka meza katika maeneo ya barabara na kwa mantiki hiyo kuzuia uingiaji wa magari makubwa sababu unakuta bado kuna shughuli za uingizaji wa mizigo mikubwa ndani ya soko.
“Nitoe rai kwamba uongozi wa wafanyabiashara ndogo ndogo eneo la Kariakoo waanze kufungua barabara hizi ili magari yatakapoanza kupita, mwisho wa siku soko litakapozinduliwa kusiwe na msongamano wa aina yoyote kuhusu kuingia ama kutoka kwa barabara za hiyo njia.
“Wafanya biashara hao wako watu watakaoniuliza watakwenda wapi, wafanyabiashara wote na hasa wafanyabiashara ndogo ndogo katika lile soko jipya ambalo limejengwa tumeratibu menejimenti ya shirika la soko Kariakoo wataeleza,
“Limeratibu kadri watakavyozidi kupanda sakafu ya kwanza kwenda mpaka ya tatu hadi ya nne kutakuwa na vijiduka vidogo vidogo ambavyo wafanyabiashara wa biashara ndogo ndogo watapangwa.
“Sasa Natoa muda wa wiki mbili ili uongozi wa Machinga katika eneo la Kariakoo waweze kukaa na wafanya biashara ndogo ndogo wawaeleze kuhusu azma ya serikali na namna ya kufungua njia ili mwisho lisije likawa soko ambalo halina tija kwa uwekezaji mkubwa ambao umeshafanywa sasa,” amesema.
Kwa upande wake Meneja Mkuu wa Shirika la Masoko Kariakoo, Ashraph Abdulkarim amesema shirika limejipanga kutangaza maeneo yaliyo wazi ili wafanyabiashara waweze kuyaomba, jambo litakalofanyika ndani ya siku saba.
Amesema wamejipanga kutangaza maeneo ya biashara yaliyowazi katika soko hilo, Juni mbili mwaka huu 2025.
“Tutatangaza maeneo hayo kwa wafanyabiashara wote na wananchi wenye nia ya kufanya biashara katika soko la Kariakoo tunawakaribisha.
“Muwe tayari ndani ya siku saba tutafanya uchambuzi wa wale watakaokuwa wamepata ili tuweze kuendelea na biashara,” amesema.
Amesema kwa wafanyabiashara waliokuwepo awali katika soko hilo kabla halijaungua wanamalizia kufanya uhakiki kwa wale ambao walikuwepo lakini wamefariki, kwa hiyo kuna taratibu za mirathi za kufuata kupitia Kamati ya mirathi.
Pia kuna maelekezo ya wale waliokuwa wanadaiwa kabla ya soko halijaungua kwa hao tunawapigia simu na kuwaelekeza tena nini cha kufanya.
Amesema sakafu ya kwanza kutakuwa na mboga mboga na kila sakafu itakuwa na biashara tofauti na nyingine, sakafu ya tatu, nne na tano kutakuwa na viuatilifu, nafaka na vifungashio.
Pia kuna maeneo ya migahawa hivyo wanaohitaji kufanya biashara hiyo wafike pindi litakapotolewa tangazo.