Na Mwandishi Wetu
DODOMA: CHAMA cha Kulinda na Kutetea Haki za Walimu Tanzania (CHAKUHAWATA) kimetangaza mafanikio 10 ndani ya kipindi cha miaka 11 tangu kuanzishwa kwake mwaka 2015.

Akizungumza jijini Dodoma katika kikao cha Kamati ya Utendaji, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Abisias Lutandika, amesema CHAKUHAWATA kilianza kikiwa na wanachama 182 pekee, lakini hadi Februari 2026 kimekua na kufikia wanachama 49,750 nchi nzima, huku zaidi ya walimu 3,000 wakiwa wamewasilisha maombi ya kujiunga.
Amesema chama kimefanikiwa kuendesha chaguzi za viongozi katika wilaya 84, huku maandalizi yakiendelea kwa wilaya 44 zilizotimiza masharti ya kikatiba.

Kwa mujibu wa Lutandika, mafanikio mengine ni pamoja na kuimarika kwa mshikamano miongoni mwa walimu na kujengwa kwa ushirikiano mzuri na Serikali kupitia majadiliano ya pamoja pindi changamoto zinapojitokeza.
Aidha, chama kimekuwa kikitoa huduma za kijamii kwa wanachama wake, ikiwemo kusaidia wagonjwa, waliokumbwa na kesi, majanga ya moto pamoja na wastaafu.
Pia kimekuwa kikisaidia shule za msingi na sekondari kwa kutoa vifaa kama mashine za kunakili, kompyuta na vifaa vya ujenzi.
Katika hatua nyingine, Mkutano Mkuu wa Januari 2025 uliridhia kuhamishwa kwa makao makuu kutoka Kigoma kwenda Dodoma ili kurahisisha uratibu wa shughuli za chama.

Lutandika ameongeza kuwa chama kimefanikiwa kutatua migogoro ya kikazi, kufuatilia stahiki za wanachama na kuendesha mikutano ya kitaifa kwa kuzingatia katiba yake.


