Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: KAMPUNI ya Ujenzi wa Mawasiliano ya China (CCCC), imetoa msaada wa vifaa vya shule pamoja na chakula katika Shule ya Msingi ya Msasani A, iliyopo Dar es Salaam.
Kiongozi wa tawi la kampuni hiyo hapa nchini, Deng Honglong amesema hayo wakati wa kukabidhi vifaa hivyo katika hafla iliyofanyika katika shule hiyo.

Amesema kampuni hiyo haijajikita pekee katika ujenzi wa miundombinu, bali pia katika kujenga mahusiano yanayovuka mipaka ya lugha na mataifa, kwa lengo la kusaidia maendeleo ya kijamii, hususan ya watoto.
Amesema, ” Ninaposimama kwenye ardhi hii ya Tanzania, nikiwaangalia watoto walioko mbele yangu, moyo wangu hujaa upendo lakini pia mzigo wa kuwajali.
“Najua kuwa katika pembe mbalimbali ambazo hatuwezi kuziona, wapo watoto wengi wanaopambana na changamoto za maisha wengine hutembea kilomita kadhaa kwenda shule, wakiwa na vitabu vilivyochakaa na penseli zilizobaki vipande,”.
Amesema CCCC kwa miaka mingi imekuwa ikijenga barabara, bandari na reli, lakini mafanikio makubwa zaidi kwao ni kuunganisha watu kwa moyo wa utu kama ilivyo kwa falsafa ya “Ujamaa” ya Tanzania.

Katika tukio hilo CCCC ilitoa vifaa mbalimbali kwa watoto yakiwemo mabegi, kompasi, madaftari na vitabu mbalimbali kwa wanafunzi wa shule hiyo.
Pia mipira, mchele, unga, mafuta ya kupikia ba zawadi nyingine nyingi.
“Tunatumaini kuwa watoto hawa watapitia vitabu hivi, kucheza kwa furaha, kula kwa kushiba, na zaidi ya yote, wajue kuwa dunia inawajali,” amesema.
Pia qmesema msaada huo hauishii kwenye vifaa tu, bali ni ishara ya urafiki wa kweli na dhamira ya kulinda ndoto za watoto wa Kitanzania.
“Nguvu ya kampuni haipimwi kwa idadi ya majengo au barabara iliyojenga, bali kwa kile inachofanya kwa watu wa nchi husika hususan watoto wanaotegemewa kuwa viongozi wa kesho,” amesema.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Msasani A, Edward Mollel, ameishukuru CCCC kwa msaada huo mkubwa ambao umezidi matarajio yao.
“Tulipowasiliana nao, tuliomba madaftari na vitabu vya kujifunzia, lakini wametuletea vitu vingi zaidi mabegi, mipira, mashine ya ‘photocopy’ na hata chakula. Tunashukuru sana,” amesema Mollel.
Qmewaomba wafadhili hao kusaidia kuboresha maktaba ya shule hiyo iwapo watapata fursa nyingine ya kushiriki.
Nao baadhi ya wanafunzi waliofaidika na msaada huo walieleza furaha yao, wakisema kuwa msaada huo utachangia kwa kiasi kikubwa kuboresha mazingira yao ya kujifunza na kuleta matumaini kwa ndoto zao za baadaye.
