Nenda moja kwa moja kwenye maudhui
November 13, 2026
Habari Author 1

Bunge La Vijana 2026 Watakiwa Kuimarisha Demokrasia Na Kutetea Hoja Kwa Staha-Kamani

Na Lucy Lyatuu,Dodoma
NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi,  Ng’wasi Kamani, amewataka vijana kutumia maarifa na uzoefu walioupata katika Bunge la Vijana 2026 kwa kuimarisha utamaduni wa demokrasia na  kuheshimu mitazamo tofauti baina yao.
Kamani amesema hayo leo, katika Ofisi za Bunge jijini Dodoma, alipokuwa Mgeni Rasmi katika hafla ya kufunga rasmi Bunge la Vijana 2026, lililowakutanisha vijana 100 kutoka  vyuo vikuu mbalimbali nchini kwa Tanzania Bara na Zanzibar.
Lengo la Jukwaa hilo ni kuwajengea uwezo katika masuala ya uongozi, demokrasia na uwajibikaji ili kuwa viongozi bora wa sasa na wa baadaye, pamoja na kuwa chachu ya mabadiliko chanya katika jamii na maendeleo ya Taifa.
Amesema Bunge hilo ni jukwaa muhimu katika kuwaandaa vijana  kujenga uwezo wa kujieleza kushawishi kujenga hoja lakini pia kuongeza uelewa aa mambo ya kijamii.
Habari Picha 14362
Ameeleza kuwa kupitia mafunzo waliyoyapata Bungeninkwa siku tano wamepata fursa ya kujifunza namna ya kuchambua changamoto zinazowakabili wananchi, kujenga na kutetea hoja zao kwa staha, kusikilizana, kujadiliana na kufikia maridhiano kwa kuzingatia taratibu na kanuni za Bunge.
Aidha  Kamani amewataka washiriki kuwa mabalozi wa maarifa waliyoyapata kwa kuyafikisha kwa vijana wengine katika maeneo wanayotoka, ili kuongeza uelewa kuhusu uongozi, uzalendo na ushiriki wa wananchi katika shughuli za maendeleo ya Taifa.
Kadhalika  amewahimiza vijana kutumia mitandao ya kijamii kwa manufaa kwa kufuatilia kurasa rasmi za Serikali kuanzia ngazi ya halmashauri hadi wizara ili kupata taarifa sahihi kuhusu fursa za ajira, uwezeshaji na maendeleo. Amewataka kuwa wadadisi, kutafuta taarifa zenye ukweli na kujenga hoja zinazotokana na uelewa sahihi badala ya kufuata maoni yasiyo na msingi.
Vilevile, amesisitiza umuhimu wa vijana kuendeleza mahusiano na mitandao waliyoijenga kupitia Bunge hilo ili kuendelea kubadilishana uzoefu, maarifa na fursa mbalimbali.
 “Nawakumbusha pia kuzingatia nidhamu, kujiamini, kuheshimu muda, kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia sheria na kanuni katika kutekeleza majukumu yenu,” amesema.
Habari Picha 14363
Kuhusu umuhimu wa Bunge hilo,  Kamani amesema lina nafasi ya pekee kwa kuwa limefanyika katika maadhimisho ya miaka 100 ya Bunge la Tanzania, akieleza kuwa programu hiyo inatarajiwa kuendelea kufanyika kila mwaka ili kuwafikia vijana wengi zaidi na kuwajengea uwezo wa kushiriki katika uongozi na maendeleo ya Taifa.
Kwa upande wake, Waziri wa Kazi, Ajira, Vijana na Uwezeshaji Zanzibar,  Ali Suleiman Ameir, amesema uwekezaji katika utu, elimu na maendeleo ya vijana ni msingi muhimu wa kujenga Taifa bora.
Ameir amesema vijana wana vipaji na karama nyingi ambazo zikiendelezwa zinaweza kuwa chachu ya maendeleo ya Tanzania, akibainisha kuwa Bunge hilo limewapa washiriki fursa muhimu ya kupata uzoefu wa kiuongozi na kujifunza misingi ya demokrasia, uwajibikaji na utawala bora.
Amewahimiza vijana kutumia maarifa waliyoyapata katika kufanya maamuzi yanayozingatia maslahi ya Taifa, kuheshimu sheria na kanuni, kujenga hoja na kutafuta suluhisho kupitia mazungumzo na maridhiano.
Amesisitiza pia umuhimu wa kuimarisha uzalendo, umoja wa kitaifa, amani, demokrasia, usawa na mshikamano, huku akiwataka vijana kuwa sauti ya pamoja inayowakilisha mahitaji na vipaumbele vya vijana wa mijini na vijijini.
Habari Picha 14364
Aidha, amesema baadhi ya hoja na hotuba zilizotolewa na washiriki, hususan hotuba ya Waziri Mkuu wa Bunge hilo la Vijana, zilikuwa na mawazo muhimu yanayoweza kuzingatiwa katika michakato ya maendeleo ya Taifa.
Mbunge wa Serengeti, Marry Surat, amewataka vijana kutambua na kuthamini uwekezaji uliofanywa na Serikali pamoja na watumishi wa Bunge katika kuwaandaa kupitia mafunzo hayo, akisisitiza umuhimu wa kuyatumia maarifa na uzoefu walioupata kwa vitendo.
Surat amesema vijana hawapaswi kusubiri hadi wapate nafasi za uongozi ndipo waanze kuleta mabadiliko, bali wana wajibu wa kuchukua hatua sasa kwa kushiriki katika kutatua changamoto zinazozikabili jamii zao badala ya kusubiri au kulaumu viongozi.
Ameongeza kuwa vijana wanapaswa kuzingatia maadili, nidhamu, uadilifu na uwajibikaji wanapotoa hoja na kushiriki katika mijadala ya masuala mbalimbali ya kitaifa, ili uwekezaji uliofanywa kwao uweze kuzaa matunda kwa kujenga kizazi chenye uelewa na uwezo wa kushiriki katika uongozi na maamuzi ya Taifa.
Habari Picha 14365
Akizungumza wakati wa kufunga rasmi Bunge hilo, aliyekuwa Spika wa Bunge la Vijana 2026, Anna Mrema, amesema sauti za vijana hazipaswi kuishia ndani ya jukwaa hilo pekee, bali zinapaswa kusikika katika jamii pana ili kuwahamasisha vijana wengine kutambua haki yao ya kutoa maoni na kushiriki katika mijadala ya maendeleo.
Mrema amewataka washiriki kuendelea kupaza sauti zao kwa kujenga hoja sahihi na kuzingatia taratibu na kanuni, huku wakiwa mabalozi wazuri watakaosambaza maarifa waliyoyapata katika vyuo na jamii zao.
Amesisitiza kuwa vijana wanapaswa kuonesha kwa vitendo matokeo ya mafunzo hayo kwa kuishi katika misingi ya nidhamu, heshima na uadilifu, akibainisha kuwa uongozi ni dhamana na huduma kwa watu, si nafasi ya kujinufaisha binafsi.
Ameongeza kuwa washiriki wanapaswa kuendelea kujiamini, kutumia fursa mbalimbali watakazozipata na kuchukua hatua zinazochochea mabadiliko chanya katika jamii zao.
Bunge la Vijana 2026 limehitimishwa kwa washiriki 100, wakiwemo wanawake 47 na wanaume 53, kukabidhiwa vyeti vya ushiriki baada ya kukamilisha mafunzo hayo, hatua inayowafanya kuwa sehemu ya historia ya maadhimisho ya miaka 100 ya Bunge la Tanzania.
Habari Picha 14366
Habari Picha 14367
Habari Picha 14368
Je, habari hii ilikusaidia?
Sambaza

Maoni 0

Hakuna maoni bado. Kuwa wa kwanza kutoa maoni!

Acha maoni

Barua pepe yako haitachapishwa. Sehemu zenye * ni lazima.