Na Lucy Ngowi
GEITA: BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imeweka mkakati mahsusi wa ununuzi wa dhahabu tokea Oktoba mwaka jana 2024, ili kuwawezesha wachimbaji wakubwa na wadogo kuuza dhahabu moja kwa moja kwa benki hiyo kwa bei ya ushindani ya kimataifa.
Ofisa kutoka Idara ya Masoko ya Fedha, Rehema Kassim amemweleza hayo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipotembelea banda la BoT katika Maonesho ya Nane ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mjini Geita,

Amesema mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa Sheria ya Madini, kifungu cha 59, kinachowataka wamiliki wa leseni za uchimbaji kuuza angalau asilimia 20 ya dhahabu yao kwa BoT.
“Wachimbaji wana motisha ya kupata punguzo la malipo ya mrabaha kutoka asilimia sita hadi nne, na ada kutoka asilimia moja hadi sifuri,” amesema Kassim.

Ameongeza kuwa BoT imewawekea wachimbaji urahisi zaidi kwa kuwa sasa wanaweza kuuza hadi asilimia 100 ya dhahabu yao kwa benki hiyo.
Uwasilishaji wa dhahabu BoT unafanyika kupitia kampuni za uchenjuaji ambazo tayari zimesaini mikataba na BoT. Kampuni hizo ni Geita Gold Refinery (GGR) ya Geita, Mwanza Precious Metals Refinery, na Isographica ya Dodoma uteuzi wa kampuni hutegemea ukaribu wa eneo la uchimbaji.
Kwa mujibu wa sheria, BoT inakusanya dhahabu kwa lengo la kuongeza akiba ya taifa ya fedha za kigeni, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uchumi wa nchi.
Kupitia maonesho haya, BoT inatoa elimu kwa wananchi kuhusu jukumu lake la msingi katika kuhifadhi akiba ya fedha za kigeni, ambapo dhahabu ni mojawapo ya nyenzo kuu.
Katika hatua nyingine, Meneja wa Idara ya Mawasiliano wa BoT, Vicky Msina, amemkabidhi Waziri Mkuu Majaliwa zawadi ya sarafu ya madini ya fedha yenye thamani ya Sh. 50,000 kama kumbukumbu.
Aidha, amemwomba Waziri Mkuu kuwa “mwalimu” wa BoT kwa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu utunzaji wa noti na sarafu.