Na Lucy Ngowi
DODOMA: MTEKNOLOJIA wa chakula kutoka Bodi ya Maziwa Tanzania, Rajilan Hillal amesema Bodi hiyo imetumia fursa ya Maonyesho ya Nane Nane Kitaifa kutoa mafunzo kuhusu ubora na usalama wa maziwa kwa wadau mbalimbali wa sekta hiyo.
Maonesho hayo yanaendelea katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.
Hillal amesema mafunzo hayo yanalenga kuwawezesha wadau kutambua maziwa salama, yasiyoharibika na yaliyo bora kwa afya ya mlaji, ili waweze kuzalisha na kusindika kitaalamu.
“Tunawafundisha pia namna ya kusindika mazao makubwa mawili yanayotumika zaidi nchini, ambayo ni mtindi wa kawaida na mtindi ulioboreshwa. Lengo letu ni kuhakikisha wananchi wanapata maziwa yaliyo salama na yaliyosindikwa kitaalamu,” amesema.
Amesema changamoto kubwa ni kutowafikia Watanzania wote kutokana na upungufu wa rasilimali, lakini amewashauri wananchi kutumia maziwa yaliyosindikwa yanayopatikana kwenye viwanda vya ndani kwa kuwa ni salama zaidi.
“Tuna jumla ya viwanda 187 vinavyosindika maziwa nchini, vikiwemo vidogo, vya kati na vikubwa. Hivyo ni muhimu wananchi waachane na matumizi ya maziwa yasiyo salama yanayouzwa mitaani, hasa yale yanayohifadhiwa kwenye vyombo visivyo rafiki kama vile machupa ya maji,” amesema.
Hillal amesisitiza kuwa matumizi ya maziwa yasiyo salama yanaweza kuhatarisha afya ya mlaji, na hivyo ni muhimu wananchi kuwa makini katika kuchagua maziwa wanayoyatumia kila siku.