Na Danson Kaijage
DODOMA: SHILINGI Bilioni 31 zimetumika kukarabati uwanja wa Benjamin Mkapa ili kuboresha sekta ya michezo.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo Tanzania ( BMT), Neema Msitha amesema hayo alipokuwa akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya baraza hilo kwa kipindi cha miaka minne ya Uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Amesema gharama hizo zimekarabati viti, ikiwa ni pamoja na kuimarisha taa za uwanjani.
Kwa upande mwingine ameelezea ujenzi wa uwanja mpya wa michezo Dodoma unaotarajiwa kuanza kujengwa hivi karibuni utakaogharimu Sh. Bilioni 310.
Pia amesema Serikali kupitia Wizara husika inaendeleza ujenzi wa viwanja vya mazoezi ikiwemo Gymkhana, Leaders Club,TIRDO, Law School na uwanja wa Farasi hadi kukamilika vitatumia Sh. Bilioni 21, hilo litafanya michezo kuhimarika zaidi.
vile vile amesema ujenzi wa uwanja mpya wa michezo Arusha utagharimu S.Bilioni 338 hadi kukamilika kwake.
pia amesema Serikali imeondoa kodi ya nyasi bandia, hali iliyosaidia uwepo wa viwanja katika ngazi za Halmshauri na kusaidia vijana wengi kushiriki katika michezo.
Katibu huyo amesema mafanikio mengine katika kipindi hiki ni pamoja na kuanzishwa kwa mfumo wa usajili wa vilabu kidijitali, hali iliyoongeza usajili wa vyama kutoka 368 kwa mwaka mmoja na nusu mpaka kufikia vyama 1,638 katika kipindi cha miaka minne.
Amesema kuwa Mchezo wa mpira wa miguu umepata mafanikio makubwa kutokana na hamasa ya goli la Mama ambayo imechochea klabu za Simba na Yanga, sambamba na timu za taifa kufanya vizuri.