Na Lucy Ngowi
MOROGORO: “BARAZA la Wafanyakazi ni chombo cha kisheria chenye dhamana ya kutimiza wajibu kama Bunge la Wafanyakazi kwa ngazi ya taasisi, pia kama ilivyo Wabunge kwa ngazi ya Majimbo maana linawakilisha mawazo ya wengi,”.
Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro Stephen Magoiga, amesema hayo alipokuwa akifungua kikao cha baraza la wafanyakazi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi ( CMA) kilichofanyika Mkoani Morogoro.

Magoiga amesema jukumu la msingi la Baraza la wafanyakazi ni kushauri menejimenti katika maeneo mbalimbali ya utekelezaji wa majukumu ambayo taasisi ina wajibika kwa umma na kujadili bajeti ya taasisi na utekelezaji wake kwa kila mwaka wa fedha.
Ameliagiza baraza hilo kufanya wajibu wake kwa ujasiri na umakini ili kulinda haki na wajibu wa wale waliowachagua kwa maslahi mapana ya Taifa.
Vile vile amewataka wajumbe wote kusoma kwa makini mkataba wa baraza hasa sehemu ya wajibu ili mara zote wanapokutana wajue wanayopaswa kuyafanya.

“Sisi kama watumishi wa Umma tunawahakikishia watanzania usalama kazini na wawekezaji watapata uhakika wa mazingira rafiki ya uwekezaji nchini,” amesema.
Pia amesema mahakama itaendelea kutoa ushirikiano wote unaohitajika ili kuhakikisha tume inatekeleza wajibu wake katika kutoa haki kwa jamii ya wafanyakazi na waajiri.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa CMA, Usekelege Mpulla, amemshukuru Jaji Stephen Magoiga na kumhakikishia kuendelea kutimiza wajibu kwa kufuata taratibu na sheria.
