Na Mwandishi Wetu
KIGOMA – KASULU: MKUU wa Mkoa wa Kigoma, Simon Sirro amesema jiografia ya mkoa huo unaopakana na nchi za Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), inaufanya kuwa eneo nyeti linalohitaji kudumisha amani kwa kila hali.
Sirro amesema hayo katika Kongamano la Amani la Kuliombea Taifa lililofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Ualimu Kasulu (TCC).
Amesisitiza kuwa amani si chaguo bali ni msingi wa maendeleo kwa wananchi wa Kigoma na Tanzania kwa ujumla.
“Bila amani, hakuna biashara ya mipakani, kilimo hakiwezi kustawi, uvuvi na biashara ndogondogo haviwezi kuendelea. Amani ni uti wa mgongo wa maendeleo,” amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Isaac Mwakisu, amewapongeza viongozi wa dini kwa ushirikiano wao na serikali katika matukio mbalimbali, na kuwataka waendelee kuwaombea viongozi ili waweze kutoa maamuzi yenye busara kwa manufaa ya wananchi.

Naye Sheikh Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Nasib Mungelwa, amesema kongamano hilo limeonesha mshikamano wa wananchi licha ya tofauti zao za kiitikadi, na kwamba hali hiyo inasaidia kuimarisha amani na umoja miongoni mwao.

Akichangia katika kongamano hilo, Askofu wa Kanisa la FPCT Jimbo la Kasulu, Shadrack Bunono, amesema viongozi wa umma wanapaswa kutumia busara na hekima katika maamuzi yao kwa manufaa ya wananchi. Aliongeza kuwa sala na maombi kwa viongozi ni msingi muhimu wa mafanikio ya wilaya hiyo.

Kongamano hilo limeandaliwa na Kamati ya Maridhiano kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, likilenga kuhimiza mshikamano, amani na maombi kwa ajili ya ustawi wa taifa.