Na Mwandishi wetu
DODOMA: ASKOFU wa Kanisa Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Central Tanganyika, Kanisa Kuu la Roho Mtakatifu, Dkt. Dikson Chilongani, ameitaka Serikali na Watanzania kwa ujumla kuitumia siku ya Ijumaa Kuu kama fursa ya kusameheana na kuacha nyuma changamoto zilizopita.
Akizungumza Aprili 3, 2026, katika ibada ya Ijumaa Kuu iliyofanyika kanisani hapo, Askofu Chilongani amesema siku hiyo, inayokumbuka mateso na kifo cha Yesu Kristo, inapaswa kuwa chachu ya upendo, umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi.
Amesisitiza kuwa viongozi wa Serikali na wa dini wanapaswa kutumia nafasi zao kuimarisha umoja wa kitaifa kwa kuondoa chuki, ubinafsi na migawanyiko isiyo na tija.

Amebainisha kuwa ni muhimu kwa viongozi hao kuonesha mfano kwa kusameheana na kuweka mazingira yatakayowezesha wananchi kuishi kwa amani.
“Tumepitia changamoto mbalimbali katika kipindi kilichopita, hivyo ni wakati wa kuziachilia na kuanza ukurasa mpya wa upendo na mshikamano kwa ajili ya ustawi wa taifa,” amesema.
Aidha, Askofu Chilongani ameeleza kuwa msamaha si wa viongozi pekee, bali ni jukumu la kila Mtanzania, kwani ni tendo la kiroho linalochangia kujenga jamii yenye maelewano na utulivu.
Katika mahubiri hayo, ameongeza kuwa taifa lenye afya linahitaji viongozi na wananchi wanaojali, wanaosikilizana na wanaoepuka chuki pamoja na ubinafsi.
Wakati huo huo, Mchungaji Adrian Mdao, akisoma somo la tano kati ya masomo saba, amesisitiza umuhimu wa kusikiliza sauti za wenye uhitaji.
Amesema baadhi ya wazazi na watumishi wa umma wamekuwa wakipuuza wajibu huo kutokana na majukumu au kutokuwa tayari kusikiliza changamoto za wengine.

Ametoa wito kwa walio na mamlaka kutumia nafasi zao kusaidia badala ya kuumiza, akisisitiza kuwa kusikiliza na kujibu mahitaji ya watu ni msingi wa kujenga jamii yenye upendo, kuaminiana na mshikamano.

