Hutibu Magonjwa Mbalimbali, TPHPA Wafunguka
Na Lucy Ngowi
MAMLAKA ya Afya ya Mimea na Viuatilifu (TPHPA), imesema mmea wa Aloe dorotheae unaopatikana nchini Tanzania pekee hutibu magonjwa mbalimbali ya binadamu na mifugo.
Meneja wa Idara ya Utambuzi wa Mimea kutoka TPHPA, Dkt. Neduvoto Mollel amesema hayo alipozungumza na Mfanyakazi Tanzania kuhusu jukumu la Kitaifa la kuhifadhi sampuli na taarifa zote za bioanuwai ya mimea ya Tanzania kupitia Kitengo cha Taifa cha Kuhifadhi ya sampuli za Mimea.
Amesema mmea huo pia kwa kizigua hujulikana kwa jina la Kikori, ambao hutumika kama kiungo muhimu kwenye pombe ya kienyeji kutokana na ladha yake chungu.
“Kutokana na manufaa ya mmea huu kwa matibabu ya binadamu, hitaji lake huongezeka siku hadi siku. Wananchi wa Kang’ata huvuna kulingana na mahitaji yao na bila kufikiria kuwa unaweza ukaisha,” amesema.
Amesema walitoa elimu kwa jamii ya eneo hilo kuhusu mmea huo kuwa ni wa kipekee katika eneo lao, hivyo wautunze.
“Tuliwapa ushauri kuacha uvunaji usio endelevu kwa kuwa utasababisha mmea huu kupotea kwenye eneo lake la asili,” amesema.
Akiuelezea mmea huo amesema unapatikana nchini Tanzania pekee.
“Haupatikani katika nchi nyingine yeyote duniani ukiwa katika maeneo ya asili. Kama upo ni kwa kupelekwa kuoteshwa kama mapambo bustanini au kwa ajili ya matumizi ya dawa majumbani.
“Aloe dorotheae ni ukoo mmoja (Aloaceae) na Aloe vera. Asili ya Aloe vera ni Rasi ya Arabia Peninsula ya kusini-mashariki ya Arabia katika Milima ya Hajar ingawaje sasa unalimwa sehemu nyingi dunia kwa ajili ya matumizi mbalimbali. Asili ya Aloe dorotheae ni Tanzania,” amesema.
Amesema nchini Tanzania Aloe dorotheae hupatikana Mkoa wa Tanga, wilaya ya Handeni katika Kata ya Kang’ata na sio penginepo.
Hukua kwenye miamba yenye udongo mdogo tu unaotokana na majani yanayooza juu ya miamba.
Amesema hadi sasa Tanzania inakadiriwa kuwa na aina takribani 14,000, kati ya hizo takriban 1500 ni aina ambazo hazipatikani popote duniani isipokuwa Tanzania.
Amesema TPHPA ina jukumu kubwa la Kitaifa la kuhifadhi sampuli na taarifa zote za bioanuwai ya mimea ya Tanzania kupitia Kitengo chake cha Taifa cha Kuhifadhi ya sampuli za Mimea.
“Inahifadhi sampuli za mimea yote ya Tanzania na Taarifa muhimu zinazoambatana na sampuli hizo.
“Zaidi ya kuhifadhi sampuli kavu, TPHPA imeanzisha bustani ya kuhifadhi mimea hadimu na yenye matumizi makubwa kwa tiba ya binadamu kwa ajili ya muendelezo wa kizazi cha mimea hiyo na kwa ajili ya matumizi endelevu ya vizazi vya sasa na vya baadae ya Watanzania,” amesema.