Na Mwandishi Wetu
ADDIS ABABA ETHIOPIA: NCHI Wanachama wa Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA), zimetakiwa kushirikiana kwa sauti moja yenye nguvu bila kujenga matabaka yoyote katika kutekeleza mkataba huo ambao utaiwezesha Afrika kujitegemea katika kuleta maendeleo ya Kiuchumi, Kisiasa na Kiutamaduni.
Aidha nchi hizo zimetakiwa kuhakikisha zinatekeleza kwa vitendo makubaliano katika mkataba huo ili kuweza kujitegemea ndani ya Afrika, kupunguza madhara ya misukosuko ya uchumi wa dunia na kuweka mikakati imara katika kuifikia ajenda 2063 ya Afrika.
Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Selemani Jafo ambaye ni Mwenyekiti wa Mkutano wa 15 wa Baraza la Mawaziri wa AfCFTA ameeleza hayo alipokuwa akifungua mkutano uliofanyika Addis Ababa nchini Ethiopia.

Katika Mkutano huo, Jaffo ameeleza jinsi Tanzania inavyochukua hatua mbalimbali katika kutatua changamoto za ufanyaji biashara chini ya AfCFTA kama ujenzi wa Reli ya Kisasa ya SGR inayounganisha Bandari ya Dar es salaam na nchi jirani.
Pia Mradi wa Bwawa la umeme la Julius Nyerere (JNHPP) wa Megawati 2115, ujenzi wa viwanja vya ndege, miundombinu ya barabara, uboreshaji wa bandari za Dar es salaam, Tanga, na Mtwara, uimarishaji wa mifumo ya kidigitali na urekebishaji wa Sera ya Biashara mwaka 2003 kuwa na toleo la 2023 inayolenga kuongeza fursa za ushiriki katika biashara kwa sekta binafsi hususani wanawake na vijana.

Amesema biashara baina ya nchi za Afrika kwa kutumia taratibu na vigezo vya AfCFTA imeanza kuongezeka ambapo Tanzania, imetoa jumla ya Vyeti vya Uasili wa bidhaa vipatazo 131 kwa Makampuni
Naye Rais wa Jamhuri ya Ethiopia, Taye Atske Selassie amesisitiza kuwa AfCFTA ni zaidi ya mkataba wa biashara bali ni chombo chenye nguvu kitakachosukuma ukuaji wa kiuchumi, kuimarisha ushirikiano kati ya nchi za Afrika.
Pia kuongeza biashara na ajira, kupunguza umasikini, kuimarisha usalama wa chakula, kukuza usawa wa kijinsia, na kuharakisha utekelezaji wa Ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika
Vilevile, Katibu Mkuu wa AfCFTA, Wamkele Mene amesisitiza nchi Wanachama kuendelea kuboresha sera, kurahisisha ufanyaji biashara na kukuza ushirikiano imara kati ya sekta za umma na binafsi.