Na Vincent Mpepo (OUT)
DAR ES SALAAM. Uongozi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) umeahidi kuendelea kuboresha mazingira ya kazi kadiri ya uwezo wa kifedha wa chuo, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kuongeza ufanisi wa kazi na mapato ya taasisi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa gari jipya la ofisi yake jijini Dar es Salaam, Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Alex Makulilo, amesema chuo kinatambua changamoto zilizopo kwenye mazingira ya kazi, na kitaendelea kuzitatua hatua kwa hatua kwa kutumia rasilimali za ndani.

Profesa Makulilo amebainisha kuwa ununuzi wa gari hilo umefadhiliwa kwa mapato ya ndani ya chuo, na aliipongeza timu yote iliyosimamia mchakato huo kwa kufuata taratibu na kuhakikisha thamani ya fedha inazingatiwa.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Huduma za Mikoa na Teknolojia za Kujifunzia, Profesa Leonard Fweja, amesema gari hilo litarahisisha majukumu rasmi ya Makamu Mkuu wa Chuo, hasa katika kusimamia vituo vya OUT vilivyopo nchi nzima.
Kwa upande wake, Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu, Dkt. Dunlop Ochieng, ametaja upatikanaji wa gari hilo kuwa ni matokeo ya mshikamano na kujituma kwa wafanyakazi wa chuo.
Benjamin Bussu, Mkurugenzi wa Mipango na Maendeleo, amesema mchakato wa manunuzi ulianza Februari 2025 na ulifuata taratibu zote, ikiwemo kupata kibali kutoka kwa Katibu Mkuu Kiongozi.
Gari lililonunuliwa ni aina ya Toyota Land Cruiser yenye thamani ya Sh. milioni 386, na linatarajiwa kuimarisha shughuli za kiutendaji za viongozi wa chuo.
Bussu amesisitiza umuhimu wa kulitunza gari hilo na kulitumia kwa uangalifu kwa maslahi ya taasisi na usalama wa viongozi wake.