Na Lucy Ngowi
GEITA: MKUU wa Wilaya ya Geita, Hashim Komba, amewataka wananchi kujenga utamaduni wa kutumia taasisi za kifedha zilizosajiliwa na kutambuliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ili kuepuka kupoteza fedha na mali kwa taasisi za kifedha zisizo rasmi.
Komba amesema hayo alipotembelea banda la Benki Kuu Tanzania katika maonyesho ya sekta ya madini yanayoendelea mkoani Geita.

Amesema matumizi ya taasisi zisizosajiliwa ni chanzo kikubwa cha malalamiko, hasara, na migogoro ya kifedha kwa wananchi.
“Natoa rai kwa wananchi kutumia taasisi zinazotambulika kisheria ili kama changamoto ikitokea, Benki Kuu na wadau wake waweze kuchukua hatua kumlinda mtumiaji,” amesema.
Ameongeza kuwa baadhi ya taasisi zisizo rasmi zimekuwa zikitumia mwanya wa kukosekana kwa usimamizi kutoa mikopo kwa riba kubwa, ambayo huishia kuwafilisi wananchi.

“Tumepokea malalamiko kutoka maeneo mbalimbali, hasa katika mji mdogo wa Katoro, ambako baadhi ya taasisi zisizotambulika zimekuwa zikiwatoza riba kubwa wananchi na hata kuwanyang’anya nyumba,” amesema.
Katika ziara hiyo, Komba pia ameelezwa kuridhishwa na ushirikiano kati ya DIB na BoT katika kulinda amana za wananchi wanaotumia taasisi rasmi.
“Kuweka fedha kwenye taasisi zinazotambulika kuna faida kubwa, kwani hata ikitokea changamoto, kuna bodi inayoshirikiana na BoT kuhakikisha fedha za wananchi hazipotei,” amesema..

Mkuu huyo wa wilaya ameonya kuwa serikali haitasita kuchukua hatua kali dhidi ya taasisi au watu binafsi wanaotoa huduma za kifedha bila usajili.
“Taasisi zinazokopesha bila usajili ni tishio. Tumechukua hatua kwa baadhi yao kwa kushirikiana na BoT kupitia kitengo chao cha uchunguzi. Tutaendelea kuwafuatilia na kuzifungia,” amesema.
Amewaonya wananchi dhidi ya tamaa ya fedha za haraka kupitia taasisi zisizojulikana, hasa zile zinazotuma ujumbe mfupi wa ofa za mikopo kwa njia ya simu.
“Kwa sasa, matapeli wanatumia teknolojia kutuma ujumbe wa mikopo ya haraka. Tuachane na tamaa hizi. Tuchague taasisi zinazotambulika ili serikali iweze kutulinda iwapo changamoto itatokea,” amesema.

Pia amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na kuwezesha sekta binafsi, jambo lililoonekana wazi kwenye maonyesho hayo.
“Mwaka jana tulikuwa na washiriki 300. Mwaka huu wamefika zaidi ya 600. Hii ni ishara kuwa sekta binafsi inakua, na juhudi za Rais Samia zina matokeo chanya,” amesema..
