Na Lucy Ngowi
GEITA: KAMPUNI ya Sotta Mining Corporation Ltd inaendelea na ujenzi wa mgodi wa kisasa wa dhahabu katika eneo la Nyanzaga, wilayani Sengerema, mkoani Mwanza, ambapo shughuli hizo zinatarajiwa kukamilika ndani ya miaka miwili, na uzalishaji wa kwanza wa dhahabu kuanza rasmi ifikapo robo ya kwanza ya mwaka 2027.
Akizungumza kuhusu maendeleo ya mradi huo, Mhandisi Mkuu wa Mradi, Richard Ojendo, amesema tayari nyumba 151 zimejengwa kwa ajili ya wananchi waliopisha mradi huo, huku nyumba nyingine 111 zikiendelea kujengwa na kukamilika ifikapo mwezi Oktoba mwaka huu.

Amesema Mradi huo pia unahusisha ujenzi wa kinu cha kuchakata dhahabu, kitakachohusisha shughuli za kusaga na kusigina, kazi ambayo pia itachukua miaka miwili.
Sotta Mining Corporation inamiliki mgodi huo kwa asilimia 80, huku Serikali ya Tanzania ikiwa na umiliki wa asilimia 20.
“Nipo hapa kusimamia mradi huu muhimu kwa taifa. Tuko hatua ya ujenzi wa miundombinu na tunaendelea kuhamasisha wananchi waliokuwa eneo hili kuupisha mradi. Tunajenga kwa viwango vya juu na kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma,” amesema Mhandisi Ojendo.

Wananchi waliopisha mradi huo wameanza kunufaika na maendeleo yanayoletwa na uwepo wa mgodi huo. Prisca Mapembe, mmoja wa waliojengewa nyumba, amesema maisha yao yamebadilika kwa kiwango kikubwa.
“Awali maisha yalikuwa duni, lakini sasa tumejengewa nyumba bora zenye hadhi, tuna maji safi na salama, umeme umefika, na visima vya maji vimechimbwa. Pia zikitokea nafasi za kazi, tunapewa kipaumbele,” amesema Prisca.

Kwa upande wake, Felician Bukwimba, mmoja wa vijana walioajiriwa katika shughuli za ujenzi, amesema mgodi huo umekuwa neema kwao.
“Ninajivunia kufanya kazi katika mradi huu. Wazawa tunapewa kipaumbele hasa kwenye kazi kama za utengenezaji wa tofali na nyinginezo. Hii ni fursa ambayo haipatikani kirahisi,” amesema Bukwimba.
Mradi wa Nyanzaga unatarajiwa kuwa moja ya migodi mikubwa ya dhahabu nchini, ukiwa na mchango mkubwa kwenye uchumi wa taifa na kubadili maisha ya wakazi wa maeneo ya jirani.