Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: MGOMBEA udiwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Haji Manara, ameahidi kuleta mageuzi ya kweli katika Kata ya Kariakoo ambayo ni kongwe na kitovu cha biashara nchini, kwa kushirikiana kwa karibu na wananchi na wafanyabiashara wa eneo hilo.
Manara ametoa ahadi hiyo alipokuwa akihutubia mkutano wa kampeni wa kata hiyo.
“Hii ni siku muhimu kwa ustawi wa Kariakoo. Nimerudi kushirikiana nanyi kujenga Kariakoo mpya, yenye maendeleo kwa wote. Kariakoo si kata ya kawaida, ni ya kipekee ni kongwe, inaongoza kwa mapato nchini, na ni kitovu cha biashara Tanzania,” amesema Manara.
Pia amesema Kariakoo ni sehemu yenye historia kubwa, ikiwa ni moja ya maeneo ambapo harakati za ukombozi wa taifa zilifanyika, na kwamba kwa CCM ni kata mtambuka inayohitaji kiongozi makini atakayeunganisha makundi yote.

“Mimi sitakuwa diwani wa wakazi pekee wala wa wafanyabiashara peke yao. Nitakuwa diwani wa watu wote Kariakoo ni yetu sote. Bila wafanyabiashara, Kariakoo itasinyaa. Maendeleo hayawezi kutokea bila wao,” amesema.
Manara ameeleza kwamba hagombei nafasi hiyo kwa ajili ya kupambana na wafanyabiashara, kwani anapenda maendeleo na anaamini wafanyabiashara ni injini ya uchumi wa Kata hiyo.
Ameahidi kuwa biashara zitaendelea kufanyika kwa uhuru na kwa saa zote za siku na usiku, kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama.
“Biashara zitafanyika hadi usiku kwa sababu si watu wote wana nafasi ya kununua mchana. Tutahakikisha tunashirikiana na polisi kudumisha usalama na kuruhusu biashara kufanyika kwa masaa mengi zaidi,” amesema.
Akigusia maendeleo yaliyofikiwa, Manara amesema miundombinu ya barabara katika Kariakoo imeboreshwa kwa zaidi ya asilimia 95, huku changamoto ya umeme ikianza kutatuliwa katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita.
“Kama umeme utakatika nikiwa diwani, mnapaswa kunipigia mimi. Mimi si kikwazo, bali ni daraja la maendeleo,” amesema.
Manara ameahidi hatawadhulumu wala kuwabughudhi wafanyabiashara wadogo, bali atahakikisha wanapewa heshima na mazingira bora ya kufanya biashara zao.
“Sitakuwa kikwazo. Nitasaidia kuwapigania wafanyabiashara wadogo wawe na hadhi yao katika jamii. Maendeleo ni kwa wote,” amesema.
Aidha, amewataka wakazi wa Kariakoo kumpigia kura yeye, pamoja na wagombea wengine wa CCM akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan, na Mgombea Ubunge wa Jimbo la Pangani, Jumaa Aweso, akisema kuwa serikali ya awamu ya sita imefanya kazi kubwa na inastahili kuendelea kupewa nafasi.
“Tumshukuru Rais Samia. Serikali imetoa Sh. Bilioni 30 kwa ajili ya maendeleo ya Kariakoo. Hospitali yetu ya Mnazi Mmoja sasa ina kipimo cha kisasa cha MRI. Haya ni mafanikio makubwa. Msimuache Mama Samia, tumpe kura za kishindo asilimia 99.9,” amesisitiza.
Pia amempongeza Mussa Zungu, kwa juhudi zake za kupigania maendeleo ya Kariakoo, akisema amekuwa mstari wa mbele kila mara kulinda maslahi ya eneo hilo.
“Zungu ni zaidi ya mzazi kwangu ni rafiki wa karibu. Kukiwa na shida Kariakoo, hata kama yuko mbali, huwa anapiga simu kushughulikia.” Amesema.
“Ni wakati wa kuchagua maendeleo. Tupige kura kwa Rais Samia, Mussa Zungu, na Haji Manara kwa pamoja tutaleta mageuzi ya kweli Kariakoo.”
Katika mkutano huo, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, ameshiriki na kutoa majibu ya moja kwa moja kuhusu changamoto ya maji na maji taka inayoikabili Kariakoo.
Aweso ameeleza kuwa serikali kupitia DAWASA na ufadhili wa zaidi ya Sh. Bilioni 200 kutoka Korea, inaendelea kutekeleza mradi mkubwa wa maboresho ya mfumo wa maji taka katika maeneo ya Kariakoo, Jangwani, Mchikichini na mengineyo.