Na Mwandishi Wetu
TUME ya Ushindani (FCC), imeshiriki Maonesho ya Biashara ya Kimataifa Barani Afrika (IATF) yanayofanyika mjini Algiers, Algeria yaliyoanza Septemba nne hadi 10, mwaka huu 2025.
Aidha maonesho hayo yanawakutanisha wawekezaji na wafanyabiashara kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika kujadili ushirikiano na fursa za biashara.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Umma wa FCC, Roberta Feruzi amesema hayo katika maonesho hayo yanayomalizika kesho Septemba 10.

Amesema katika maonesho hayo FCC inatoa elimu kuhusu ushindani na ushajishaji wa uchumi kwenye soko nchini Tanzania.
Amesema jukumu la tume hiyo ni kuwaeleza wawekezaji kuwa Tanzania ni soko salama na lenye uwazi na ushindani wa haki.
“Tunatoa miongozo kwa wadau wanaotaka kushirikiana na kampuni za ndani katika kununua au kuungana kibiashara na tunarahisisha mchakato mzima.
“Kupitia ushiriki wake, Tanzania inalenga kutumia IATF kama jukwaa la kutangaza fursa, kuimarisha urahisi wa uwekezaji na kufungua milango ya ushirikiano wa kibiashara barani Afrika,” amesena.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Suleiman Serera, ameongoza ujumbe wa Tanzania akiwa na Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Iman Njalikai, wametembelea Banda la Tanzania na kujadiliana na wawekezaji kuhusu fursa zilizopo nchini.
![]() |
Mbali na FCC, taasisi nyingine kutoka Tanzania zinazoshiriki katika maonesho hayo ni pamoja na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE, Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Eneo Maalum la Uwekezaji Tanzania (TISEZA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA).
Pia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na Mamlaka ya Ukuzaji Uwekezaji Zanzibar (ZIPA).