Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amelipongeza Jeshi la Magereza kwa hatua kubwa ya kurasimisha ujuzi wanaoupata wafungwa kupitia Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), hali inayowawezesha kupata ajira au kuanzisha shughuli za kujitegemea baada ya kumaliza vifungo vyao.
Ametoa pongezi hizo wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka 64 ya kuanzishwa kwa Jeshi la Magereza, yaliyofanyika katika viwanja vya Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania kilichopo Ukonga, jijini Dar es Salaam.

“Ninatoa pongezi za dhati kwa Jeshi la Magereza kwa mafanikio haya. Huu ni mpango kazi wenu na tumeona faida zake. Vijana waliokuwa hapa wametoa ushuhuda namna walivyonufaika na mafunzo haya ya stadi za kazi.” amesema.
Ameeleza kuwa kupitia mitaala mipya ya mafunzo ya amali na stadi za kazi, Jeshi hilo limefanikiwa kuwafikia na kunufaisha zaidi ya wafungwa 5,000, ambapo baadhi yao tayari wamepata ajira au wameanzisha biashara binafsi baada ya kutoka gerezani.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sagini amelipongeza Jeshi hilo kwa umahiri wake wa kutafsiri na kutekeleza maelekezo ya Serikali pamoja na viongozi mbalimbali, hata mara nyingine bila kuwezeshwa kifedha moja kwa moja kutoka serikalini.
Sagini amesema Jeshi la Magereza limeendelea kufanyia kazi mapendekezo ya Tume ya Rais ya Maboresho ya Vyombo vya Haki Jinai, ikiwa ni pamoja na kuboresha programu za urekebishaji wa wafungwa.
“Ujuzi wanaoupata wafungwa kupitia mafunzo haya ni wa muhimu sana katika kuwawezesha kufanya shughuli halali za kujikimu mara baada ya kurudi kwenye jamii, na hivyo kusaidia kupunguza uwezekano wa kurejea katika makosa.” amesema.

Awali Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, Jeremiah Katungu, ameeleza kuwa Jeshi hilo limefanikiwa kuandaa mitaala mipya 10 kwa ajili ya kuboresha utoaji wa mafunzo stahiki kwa watumishi wake na kwa wafungwa.
Mitaala hiyo imeandaliwa kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali zikiwemo Chuo cha Ustawi wa Jamii, Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), pamoja na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW).
“Tumeandaa pia Mwongozo wa Programu za Urekebishaji kwa Wafungwa. Mwongozo huu umeweka misingi thabiti na utaratibu wa mapokezi, tathmini, urekebishaji, pamoja na kuwaandaa wafungwa kurejea kwenye jamii wakiwa raia wema,” amesema.