Na Lucy Ngowi
Aiomba Serikali Kusaidia Vyama Vya Wafanyakazi
ARUSHA: MAKAMU wa Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Shabani Mwabungulu amesema shirikisho hilo litaendelea kushirikiana na serikali katika kuimarisha ustawi wa wafanyakazi na uchumi wa taifa kwa ujumla.

Amesema hayo alipokuwa akitoa salamu za shukrani kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete katika hafla ya uzinduzi wa jengo la biashara la TUCTA, jijini Arusha.
Mwabungulu amesema ujenzi wa jengo la kisasa la TUCTA siyo tu utaimarisha shughuli za shirikisho hilo, bali pia utachangia pato la serikali kupitia kodi.

“Kupitia jengo hili, tutaweza kujiendesha kwa ufanisi zaidi na wakati huo huo kuchangia mapato ya serikali. Hii ni sehemu ya dhamira yetu ya kuwa wabia wa maendeleo ya taifa,” amesema.
Ametoa wito kwa serikali kuendelea kushirikiana na TUCTA kwa kusaidia kuviimarisha na kuvisimamia vyama vya wafanyakazi ili viwe na uwezo wa kutetea maslahi ya wanachama wao kwa ufanisi zaidi.

“Tunaomba usaidizi wa serikali katika kuboresha mazingira ya uendeshaji wa vyama vyetu. Ushirikiano huu ni muhimu kwa mustakabali wa haki na maendeleo ya wafanyakazi nchini,” amesema.
