Na Lucy Ngowi
ARUSHA: RAIS wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Tumaini Nyamhokya, amesema ni nadra kukuta vyama vya wafanyakazi vikimiliki mali yenye thamani kama wanayomiliki sasa.

Nyamhokya amesema hayo katika hafla ya uzinduzi wa jengo jipya la biashara jijini Arusha, lililozinduliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu),
“Miaka ya nyuma, mwajiri akisikia viongozi wa vyama wanakuja, aliona kama ni vita. Lakini viongozi tuliopo sasa, tangu 2017, tulikubali kubadilika tumeamua kutumia njia ya majadiliano na serikali.” amesema Nyamhokya.

Amesema kupitia usimamizi wa kisasa na ushirikiano na taasisi za serikali, TUCTA imeweza kukarabati mali nyingi zilizokuwa zimechakaa, ikiwa ni pamoja na chuo chao kilichoko Mbeya, nyumba kubwa jijini Dodoma, na sasa jengo hilo la biashara jijini Arusha.
“Katika jengo hilo la biashara kuna huduma mbalimbali ikiwemo hoteli, maduka ya vifaa vya magari, vitabu, nguo za wanawake, wanaume na watoto, pamoja na bidhaa mchanganyiko hatua iliyolenga kuinua mapato ya shirikisho na kutoa ajira,” amesema.

Kwa upande mwingine amesema, Kwa sasa, shirikisho hilo lina vyama 16, kutoka vyama 13 vya awali.
Amevitaja vyama vipya vilivyopokelewa ni pamoja na Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari (JOWUTA), Chama cha Wafanyakazi wa Sekta ya Ulinzi Binafsi (TUPSE) na Chama cha Wafanyakazi wa Huduma za Viwandani Tanzania (TASIWU).

Pia amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia nyongeza ya mishahara kwa wafanyakazi wa umma iliyotolewa Julai mwaka huu, kama alivyoahidi katika sikukuu ya Wafanyakazi ijulikanayo kama Mei Mosi mwaka huu 2025.
“Mama ameonyesha upendo kwa wafanyakazi. Aliahidi, ametekeleza. Sasa tunajisikia salama. Ni nafuu kuwa na kiongozi anayesikiliza unagonga mlango, anafungua,” amesema.

Pia amemshukuru Waziri Ridhiwani kwa kuendelea kushirikiana nao kwa karibu. “Tunakuombea uchaguzi uende salama na Rais Samia akupange katika wizara hii hii. Umeonesha dhamira ya kweli kwa wafanyakazi,”.
Katika kudumisha mshikamano, TUCTA imeandaa vyeti maalum kwa ajili ya vyama vyote vya wafanyakazi, ikiwa ni njia ya kutambua mchango wao katika maendeleo ya shirikisho hilo.