Na Lucy Ngowi
MOROGORO: TAASISI ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), imesema kuwa tafiti zinazofanyika zimejikita kupunguza athari za visumbufu mbalimbali vikiwemo vya hali ya hewa kama ukame, joto la kupita kiasi, rutuba hafifu, visumbufu vya kibaiolojia kama wadudu, magugu na magonjwa.
Mkurugenzi wa TARI Ilonga iliyopo Kilosa Morogoro, ambaye pia ni Msimamizi wa Mahindi nchini, Dkt. Arnold Mushongi, amesema hayo katika Maonesho ya nanenane Kanda ya Mashariki.

Amesema TARI Ilonga imebuni teknolojia zinazoongeza uhimilivu wa uzalishaji katika mazingira changamoto, ili kuhakikisha kuwa mkulima anapata mavuno mengi kupitia mbegu bora na za kisasa.
Amesema Programu ya utafiti wa mahindi ni kubwa kuliko zote kutokana na umuhimu wa zao hilo, ambalo siyo tu ni chakula kikuu kwa Watanzania, bali pia ni zao la biashara linalotoa mchango mkubwa kwa taifa kupitia fedha za kigeni, viwanda, na ajira.

“Mahindi ni zao pana linalofanyiwa tafiti nyingi kutokana na matumizi yake mbalimbali.
“Hata hivyo, Tanzania bado haijalitendea kazi ipasavyo. Rais Samia Suluhu Hassan, amesisitiza kuwa Tanzania inaweza kulisha Afrika, na mahindi ni zao kuu katika kufanikisha azma hiyo,” amesema.
Amesema mahindi mengi ya ziada yanauzwa nje ya nchi kutokana na kuwepo kwa soko kubwa. Uwezo wa taifa kuzalisha mahindi ni tani milioni 18 kwa mwaka, lakini bado tupo kwenye theluthi moja ya kiwango hicho.
Amesema Kitafiti, maeneo ya uzalishaji yamegawanywa katika uwanda wa joto, uwanda wa kati na uwanda wa juu kwa ajili ya kufanya tafiti sahihi kulingana na mazingira.
Changamoto nyingine kubwa ni upotevu baada ya mavuno licha ya kuzalisha tani milioni saba kwa mwaka.
Kwa miaka mingi, juhudi zimekuwa zikielekezwa kwenye kuongeza uzalishaji, lakini sasa tunasisitiza pia kulinda ubora wa mazao baada ya kuvunwa.
Dkt. Mushongi anasisitiza kuwa serikali iwekeze zaidi kwenye tafiti zinazolenga kupunguza pengo hilo, ili kuhakikisha kuwa kinachozalishwa kinabaki na ubora unaokusudiwa hadi sokoni.