Na Lucy Ngowi
MOROGORO: KATIKA juhudi za kuongeza uzalishaji wa mafuta ya alizeti nchini, Serikali kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) imewekeza katika utafiti wa mbegu bora za alizeti zitakazosaidia wakulima kuongeza tija mashambani.
Kwa mujibu wa Mtafiti Msaidizi kutoka TARI Ilonga, Daniel Mashati, taasisi hiyo imefanikiwa kuendeleza aina tatu bora za mbegu za alizeti ambazo ni Record, TARI NAL 2019, na TARI ILO 2019.

Mashati amesema mbegu hizo ni za aina ya chavua na zimeonyesha uwezo mkubwa wa kutoa mazao mengi endapo mkulima atazingatia kanuni bora za kilimo.
Akizungumzia kuhusu nafasi ya upandaji, Mashati amesema kuwa kwa mbegu ndefu kama Record na TARI NAL 2019, mkulima anapaswa kupanda kwa nafasi ya sentimita 75 kati ya mstari na mstari, na sentimita 30 kati ya mche na mche.
Kwa upande wa mbegu fupi kama TARI ILO 2019, nafasi sahihi ni sentimita 60 kati ya mstari kwa mstari, na sentimita 30 kati ya mche kwa mche.

Amesema bado mahitaji ya mafuta ya kula nchini ni makubwa kuliko uzalishaji wa ndani, hali hiyo imeilazimu serikali kuendelea kuwekeza katika tafiti za mbegu bora ili kuhakikisha wakulima wanapata mbegu zenye ubora, zinazotoa mavuno mengi na hivyo kusaidia kupunguza uagizaji wa mafuta kutoka nje ya nchi.