Wakulima Wafaidika na Mapato Yaongezeka
Na Lucy Ngowi
DODOMA: MKOA wa Dodoma umeendelea kung’ara katika utekelezaji wa mfumo wa stakabadhi ghalani, ambapo zaidi ya tani 1,000 za mazao ziliuzwa kupitia mfumo huo.
Mrajis wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Dodoma, Joseph Chitinka amesema leo katika viwanja vya maonesho vya Nanenane Nzuguni Dodoma.

Amesema mafanikio hayo yamewanufaisha wakulima kwa kuongeza kipato chao, huku serikali ikipata mapato ya kutosha kutokana na shughuli hizo.
Amesema mfumo huu umeleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi kwa wakulima wadogo ambao sasa wanaweza kuuza mazao yao kwa bei nzuri na kwa uhakika.
“Tumeweza kufanya transformation ya maisha hasa ya wakulima wadogo kutoka hatua moja kwenda nyingine,” amesema.
Amesema Mkoa wa Dodoma una jumla ya vyama 126 vya ushirika, ambapo kati ya hivyo, 27 vinajihusisha moja kwa moja na kilimo. Pia, kuna zaidi ya SACCOs 70 zinazojumuisha zile za mahala pa kazi pamoja na za kijamii zinazowahudumia wananchi wa kawaida, wajasiriamali, na wafanyabiashara.
“Mkoa huu umeendelea kuimarika katika uzalishaji wa mazao matano makuu ambayo ni ufuta, choroko, mbaazi, dengu na zabibu.
“Zabibu inatajwa kuwa ni zao la kipekee na fahari ya mkoa huo. Wadau wa zao hilo wamefanikiwa kuongeza thamani kwa kutengeneza bidhaa mbalimbali kama mchuzi wa zabibu kwa ajili ya kutengeneza wine,” amesema..
Amesema hadi sasa, kuna viwanda viwili vinavyoongeza thamani ya zabibu mkoani Dodoma.
Amesema mchuzi wa zabibu umevutia soko kubwa, ikiwemo kwa wafanyabiashara wakubwa wanaousafirisha hadi nje ya nchi kwa ajili ya kutengeneza wine.
Katika maonyesho ya mwaka huu, vyama vya ushirika vya zabibu vimeshiriki kikamilifu na kuuza bidhaa zao kwa wingi, jambo lililowawezesha kupata kipato na kuimarika kiuchumi.
Aidha, mkoa wa Dodoma umeanza maandalizi ya ukusanyaji wa mazao ya mbaazi, choroko na dengu kwenye maghala mbalimbali, na minada inatarajiwa kuanza katikati ya mwezi huu.
Chitinka amesema ushirika wa kuweka na kukopa umekuwa sehemu muhimu ya maendeleo ya kiuchumi ya wakazi wa Dodoma, ambapo SACCOs mbalimbali zimeweza kutoa mikopo kwa wanachama, kuwainua wajasiriamali na wafanyabiashara, na kuhamasisha watu zaidi kujiunga na vyama vya ushirika.