Na Lucy Ngowi
DODOMA: KAMPUNI ya Mbolea Tanzania (TFC) imeweka mikakati ya kusimika kiwanda kikubwa cha kuchanganya na kuzalisha mbolea nchini, kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa ndani na kupunguza utegemezi wa mbolea kutoka nje.
Mkurugenzi Mkuu wa TFC, Samwel Mshote amesema kampuni hiyo inatarajia kupokea mitambo maalum kwa ajili ya mradi huo, na tayari imepata mbia kutoka Zambia ambaye atashiriki katika uwekezaji.
Amesema Kiwanda hicho kitalenga kuzalisha mbolea kwa kuzingatia mahitaji halisi ya udongo katika maeneo mbalimbali ya Tanzania.

Amesema Kiwanda kitategemea rasilimali zinazopatikana hapa nchini, ikiwemo makaa ya mawe na madini ya phosphate kutoka mikoa ya Manyara na Songwe.
“Kwa sasa, TFC imepatiwa ardhi yenye ukubwa wa ekari 2,750 katika Manispaa ya Tabora kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda hicho. maandalizi ya awali yameanza, na ujenzi unatarajiwa kuanza ndani ya mwaka huu,” amesema.
Amesema hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za serikali kufanikisha uzalishaji wa mbolea ndani ya nchi, kupunguza matumizi ya fedha za kigeni, pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia ajira mpya na kuongeza kipato cha wananchi.
Wakati huohuo, TFC imejiandaa kusambaza jumla ya tani 200,000 za mbolea kwa msimu huu.
Amesema mbolea zitakazosambazwa ni pamoja na aina ya Diammonium Phosphate (DAP), Urea (N-46), na Calcium Ammonium Nitrate (CAN 27), ambapo usambazaji wa DAP na Urea tayari umeanza kufanyika katika maeneo mbalimbali ya nchi, huku shehena nyingine zikiwa bionic kusambaziwa.
Aidha, TFC inaendelea kupanua mtandao wake wa mauzo kupitia vituo vilivyopo katika mikoa ya Mbeya, Njombe, Rukwa, Ruvuma, Mwanza na Tabora. Kampuni hiyo inawahamasisha Watanzania kushiriki katika mnyororo wa usambazaji wa mbolea kwa kujitokeza kuwa mawakala katika maeneo yao.