Na Lucy Ngowi
DODOMA: MAMLAKA ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), imeendelea kutoa elimu kuhusu njia bora, salama na rafiki kwa mazingira za kudhibiti visumbufu vya mazao.
Mojawapo ya njia hizo ni matumizi ya ndege wa aina ya bundi kwa ajili ya kudhibiti panya mashambani.
Ofisa Kilimo kutoka TPHPA, Mathias Bernard ametoa elimu hiyo katika Maonesho ya Nanenane ya Kitaifa na Kimataifa yanayoendelea mkoani Dodoma.

Amesema jitihada zote hizo zinafanywa na TPHPA kuhakikisha wakulima wanapata mazao bora kwa tija,
Amesema katika maonesho hayo, TPHPA imekwenda na suluhisho la kipekee ambalo linatumia teknolojia ya asili katika kukabiliana na changamoto sugu ya panya kwenye mashamba ya wakulima wadogo na wa kati.
Amesema Kituo cha Kudhibiti Baa la Panya Morogoro ni sehemu ya mpango wa kitaifa wa kudhibiti viumbe waharibifu wa mazao kama panya na jamii zake, ambao husababisha hasara kubwa kila mwaka kwa wakulima nchini.
“Lengo letu katika kushiriki maonesho haya ni kuwaelimisha wananchi kuhusu aina mbalimbali za panya wanaopatikana katika mazingira yao, madhara wanayosababisha na njia mbalimbali za kisasa na za asili za kuwadhibiti,” alisema Bernard.
Amesema kwa muda mrefu wakulima wamekuwa wakitegemea sumu na mitego ya kawaida, lakini sasa TPHPA inahamasisha matumizi ya mbinu za kibaiolojia, ikiwemo kutumia ndege aina ya bundi, ambao ni maadui wa asili wa panya.
Amesema bundi ni ndege anayewinda usiku, na chakula chake kikuu ni panya.
“Tunashauri wakulima watengeneze viota vya bundi na kuviweka kwenye miti inayopakana na mashamba yao. Hii huwavutia bundi kuja kutaga na kuishi humo. Watoto wa bundi wakikua, huanza kutoka usiku kutafuta chakula na chakula chao ni panya,” amesema.
Amesema kwa wastani, bundi mmoja anaweza kula panya wasiopungua watatu kwa siku.
Amesema mbinu hiyo siyo tu inapunguza gharama za kudhibiti visumbufu, bali pia inalinda afya ya binadamu, ardhi, na mazingira dhidi ya madhara ya sumu kali ambazo mara nyingi hutumika bila tahadhari.
Amewashauri wakulima nchini kuanza kutumia njia hiyo ya asili kama sehemu ya mikakati ya kudumu ya kudhibiti panya.
Amesema kuwa mbali na bundi, kuna njia nyingine za kibaiolojia na kimazingira zinazofaa kutumiwa sambamba ili kupata matokeo bora.
“Kwa kutumia bundi, wakulima wanapunguza matumizi ya sumu, wanatunza mazingira, na kuongeza tija ya uzalishaji. Hii ni teknolojia rafiki kwa kila mkulima,” amesema.