Na Danson Kaijage
DODOMA: Zaidi ya asilimia 70 ya wanafunzi waliokatisha masomo kutokana na mimba katika Mkoa wa Geita wamerudi shule kuendelea na masomo, ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Takwimu hizo zimetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigela, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) jijini Dodoma, wakati akiwasilisha mafanikio ya mkoa huo katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia.

Shigela amesema kuwa mwaka 2021 wanafunzi waliorejea shuleni baada ya kupata ujauzito walikuwa asilimia 30 pekee, lakini kufikia mwaka 2025 idadi hiyo imeongezeka hadi kufikia asilimia 70.
“Hii inaonesha dhamira ya kweli ya Serikali katika kuhakikisha kila mtoto wa kike anapata haki ya elimu bila kujali changamoto alizokumbana nazo,” amesema
Ameongeza kuwa mafanikio hayo ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya elimu jumuishi inayolenga kumpa kila mwanafunzi nafasi ya pili, sambamba na kampeni za uhamasishaji zinazofanywa na viongozi wa mkoa, jamii na mashirika ya kiraia.

Katika sekta ya afya, amesema upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vifungashio umefikia asilimia 90, hatua inayotokana na maboresho makubwa yaliyofanywa katika kipindi cha miaka minne iliyopita.
Akiuelezea Mkoa wa Geita kama mkoa mchanga lakini unaoonyesha kasi ya ukuaji, Shigela amesema Geita sasa ni miongoni mwa mikoa 10 bora nchini kwa ukuaji wa pato la ndani na ongezeko la watu.
“Geita ni mkoa wa saba kwa ukusanyaji wa mapato ya ndani licha ya kuwa na miaka 12 tu tangu kuanzishwa kwake,” amesema.
Kuhusu kilimo, Shigela amebainisha kuwa serikali imeanza kusambaza vifaa vya kisasa vya kupima afya ya udongo kwa wakulima, jambo litakalowasaidia kulima kwa tija na kuendana na mahitaji halisi ya ardhi husika.