- Wagombea Watakiwa Kuvuta Subira
Na Danson Kaijage
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimeahirisha rasmi mchakato wa kuwateua wagombea wa nafasi za ubunge na udiwani, mchakato uliokuwa umepangwa kufanyika leo Julai 19, sasa ukisogezwa mbele hadi Jylai 28, mwaka huu 2025.
Taarifa hiyo imetolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Itikadi na Uenezi, Amos Makala alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo.
Ameeleza kuwa hatua hiyo imechukuliwa ili kutoa muda wa kutosha kwa chama kufanya uchambuzi wa kina kwa kila mgombea kutokana na idadi kubwa ya waliotangaza nia ya kugombea nafasi hizo.
“Tumelazimika kusogeza mbele ratiba hii kwa sababu ya wingi wa waombaji. Tunataka tuhakikishe tunafanya kazi ya uchambuzi kwa makini, kwa haki na kwa kuzingatia sifa stahiki za wagombea wote,” amesema.
Kwa mujibu wa Katibu huyo, kabla ya kufanyika kwa kura za maoni mnamo Julai 28,, kutatanguliwa na vikao muhimu vya uongozi wa juu wa chama.
Kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kinatarajiwa kufanyika Julai 26 , na siku hiyo hiyo kufuatiwa na kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho.
Aidha, Makala amewataka wagombea wote waliokwisha tangaza nia kuwa watulivu na kuendelea kufuata taratibu za chama huku wakijiepusha na kampeni za mapema au vitendo vya uchochezi vinavyoweza kuvuruga utaratibu wa chama.
“Ni vyema wagombea wakaonesha uvumilivu na nidhamu ya hali ya juu. CCM ni chama kinachoongozwa na misingi ya haki, hivyo kila mtu atapata nafasi yake ya kusikilizwa kwa mujibu wa kanuni,” amesema.
Kwa sasa, chama hicho kinasisitiza kuwa kinaendelea na kazi ya kuhakiki majina ya waombaji wote katika ngazi mbalimbali, kuhakikisha wagombea watakaopitishwa ni wale wenye uwezo, uadilifu na wanaokubalika kwa wananchi.