Na Danso Kaijage
UONGOZI wa Rais Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha miaka minne, katika Mkoa wa Mara umeonesha mageuzi makubwa kwenye nyanja mbalimbali hususan usalama, afya na elimu, mambo yanayogusa moja kwa moja ustawi wa jamii.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evance Mtambi amesema hayo alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma katika ukumbi wa Idara ya Habari-MAELEZO,.

Amesema hatua zilizopigwa katika kipindi hicho zimeimarisha maisha ya wananchi na kupunguza changamoto ambazo kwa muda mrefu ziliwakabili wakazi wa mkoa huo.
Amesema usalama katika mkoa huo, hasa kwenye maeneo ya mipakani, umeimarika kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma kutokana na ushirikiano baina ya vyombo vya dola, pamoja na elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa amani zimesaidia kudhibiti matukio ya uhalifu na biashara haramu mpakani.
“Katika miaka ya nyuma kulikuwa na changamoto za usalama katika mipaka yetu, lakini kupitia juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita, hali sasa ni tulivu. Wananchi wanafanya shughuli zao bila hofu, na hiyo inachangia uchumi wa eneo letu kukua,” amesema.
Katika sekta ya afya, Mkuu huyo wa mkoa amesema kuwa hospitali kubwa na ya kisasa imejengwa, ikiwa ni sehemu ya kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa Mara na hata wageni kutoka mataifa jirani.
“Hospitali hii si tu inahudumia wananchi wa Mara, bali pia imeandaliwa kwa viwango vya kimataifa kiasi cha kupokea wagonjwa kutoka nje ya nchi. Hili ni jambo la kujivunia,” amesema.
Kwa upande wa elimu, Mtambi ameeleza shule mpya zimejengwa na ukarabati mkubwa wa miundombinu ya zamani kufanyika.
Ametaja pia ongezeko la walimu na vifaa vya kujifunzia kuwa miongoni mwa mafanikio muhimu yaliyofanikishwa kwa juhudi za serikali.

Aidha, amesisitiza kuwa sekta ya kilimo na ufugaji imekuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo ya kiuchumi katika mkoa huo, Kupitia uwekezaji katika pembejeo bora, elimu ya kisasa kwa wakulima na wafugaji pamoja na masoko ya uhakika.
“Wananchi sasa wanaona kilimo na ufugaji kama biashara, si kazi ya kujikimu tu. Hii ni hatua muhimu kwa mkoa wetu na kwa taifa kwa ujumla,” amesema.