Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: KAMISHNA wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Nyanda Shuli amepongeza Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCPD) kwa kutekeleza kwa vitendo mapendekezo ya mabadiliko ya sheria mbalimbali yanayopendekezwa na wananchi kupitia taasisi na wadau wa haki nchini.

Akizungumza jijini Dar es Salaam alipotembelea banda la OCPD katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa yajulikanayo kama Sabasaba yanayoendelea mkoani Dar es Salaam, Kamishna Shuli amesema kazi inayofanywa na ofisi hiyo ni msingi muhimu wa kuhakikisha sheria zinakidhi mazingira halisi ya sasa.
“Ofisi hii inatoa huduma zinazoshabihiana na zetu. Tunapokea maoni ya wananchi kuhusu sheria mbalimbali ambazo zimepitwa na wakati au hazizingatii hali halisi.
“Kwa kawaida, mapendekezo hayo hupitia mchakato mrefu lakini mwisho wa safari huletwa kwenu kwa ajili ya kuandikwa upya au kurekebishwa kabla ya kuwasilishwa bungeni.
“Hii ni hatua muhimu ya kuhakikisha haki na sheria zinakwenda na wakati,” amesema.

Akitolea mfano, Kamishna ameeleza changamoto iliyobainishwa na Jaji Mfawidhi wa Kanda ya Kusini wakati wa uchunguzi uliofanywa mikoani, ambapo sheria ya Uhujumu Uchumi ilionekana kutoendana na mazingira halisi ya maeneo hayo.
Sheria hiyo iliwahusisha wanyama kama swala na digidigi katika makosa ya uhujumu uchumi, hali iliyowafanya wananchi wengi kufungwa bila dhamana kwa makosa yasiyostahili adhabu kali kiasi hicho.
“Ni jambo la faraja kwamba baada ya mchakato mrefu wa ukusanyaji maoni, sheria hiyo sasa imefanyiwa marekebisho kwa kuzingatia uhalisia na malengo halisi ya kulinda wanyama waliolengwa awali, yaani ‘Big Five’. Hili ni zao la kazi kubwa inayofanywa na Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria,” amesena.
Kwa upande wake, Mwandishi wa Sheria kutoka OCPD, Happyphania Luena, ametoa shukrani kwa Kamishna Shuli kwa kutembelea banda hilo na kutambua kazi ya ofisi hiyo, akisema kuwa ushirikiano kati ya OCPD na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ni wa mfano na wenye tija kubwa katika kulinda haki na usawa wa kijamii.
“Mbele yako ni Juzuu za Sheria zilizofanyiwa Urekebu toleo la mwaka 2023. Tumezileta hapa kuwaonesha wananchi kazi hii muhimu ya kuhuisha sheria.
“Toleo la mwaka 2002 lilifutwa rasmi baada ya Rais Samia Suluhu Hassan, kuzindua rasmi toleo hili jipya. Wananchi wanapaswa kuelewa kuwa sheria ni nyenzo ya maendeleo na si kikwazo,” amesema.
Mchakato wa urekebishaji wa sheria unatajwa kuwa chachu ya uboreshaji wa mifumo ya kisheria nchini, na unaonesha kwa vitendo dhamira ya Serikali kuhakikisha haki, uwajibikaji, na utawala bora vinazingatiwa katika kila hatua ya maisha ya wananchi.