Na Danson Kaijage
MKUU wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga amezindua rasmi zoezi la ugawaji wa mitungi ya gesi kwa bei ya ruzuku.

Uzinduzi huo umefanyika katika viwanja vya stendi ya zamani mjini Katesh, wilaya ya Hanang, ambapo jumla ya mitungi 3,000 imetolewa kwa wananchi kwa bei nafuu ya Sh. 17,500 kwa kila mtungi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Sendiga amesema mpango huo ni sehemu ya kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, hasa kwa kaya za kipato cha chini.
Ameeleza kuwa mkoa mzima wa Manyara utapatiwa jumla ya mitungi 16,275 katika mpango huo wa ruzuku.
“Nia ya serikali ni kuhakikisha kila mwananchi anapata fursa ya kutumia nishati salama na rafiki kwa afya na mazingira.

“Hili pia litasaidia kupunguza matumizi ya kuni na mkaa ambayo yanaharibu mazingira na kuhatarisha afya,” amesema.
Amewaagiza Wakuu wa Wilaya wote kuhakikisha kuwa zoezi hilo linasimamiwa kikamilifu ili kuzuia mianya ya udanganyifu na ulanguzi.

“Hatutavumilia wafanyabiashara watakaojaribu kuongeza bei kinyume na makubaliano. Bei ya mtungi ni Sh. 17,500 kama ilivyopangwa,” amesema.
Sendiga ameipongeza Serikali kwa juhudi za dhati za kulinda mazingira na kuboresha maisha ya wananchi kupitia matumizi ya nishati mbadala.

Amesema kuwa ruzuku hiyo ni chachu ya kuhamasisha mabadiliko ya tabia kutoka matumizi ya kuni na mkaa kuelekea upishi salama unaotumia gesi.