Na Lucy Lyatuu
CHUO Cha Taifa Cha Usafirishaji (NIT) kimewataka wananchi kuwaamini wana uwezo , Ujuzi na Vifaa vya kutosha Kutoa Kozi ya urubani ambayo inatolewa chuoni hapo.
Kimesema mara nyingi watu huwa wanahoji kama Chuo kimejiandaa vya kutosha kuweza Kutoa Kozi hiyo.
Akizungumza katika banda la NIT kwenye Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba, Mkufunzi wa Urubani kutoka chuo hicho, Ashrafa Ramadhan, amesema tayari mafunzo hayo yameanza na wanafunzi wa kwanza kumi wamejiunga, wakiwemo wanawake wanne na wanaume sita.
“Napenda kuwaondoa hofu. Tumejipanga ipasavyo. Tuna vifaa vya kisasa vya kufundishia marubani kabla hawajapanda ndege, na ndege mpya kwa ajili ya mafunzo zipo tayari,” amesisitiza.
Ameongeza kuwa NIT imewekeza katika miundombinu na teknolojia ya kisasa ili kuhakikisha wanafunzi wanapata mafunzo bora ya kitaalamu na ya kimataifa huku gharama zikiwa nafuu ikilinganishwa na vyuo vya nje ya nchi.
“Wito wangu kwa vijana ni kuchangamkia fursa hii adhimu. Mafunzo haya yana nafasi kubwa ya ajira na ujasiriamali katika sekta ya usafiri wa anga. Wazazi pia wawaunge mkono watoto wao kuingia kwenye fani hii ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikitawaliwa na wageni,” amesema.
Amesema NIT kinatoa rasmi mafunzo ya urubani kwa vitendo kwa vijana wa Kitanzania, huku kikisisitiza kuwa kina vifaa vya kisasa na wataalamu waliobobea katika nyanja hiyo.
“Nawakaribisha vijana kufika kwenye banda letu wapate elimu ya kina kuhusu kozi ya urubani. Mimi ni miongoni mwa wakufunzi kumi waliopo, na tumeshaanza rasmi mafunzo ya urubani chuoni kwetu. Tumejipanga vizuri kuanzia hatua za awali za kufundisha ardhini hadi mafunzo ya angani,” amesema.
Amebainisha kuwa sifa za kujiunga na mafunzo hayo ni kuwa na elimu ya angalao kidato cha nne, na umri wa kuanzia miaka 17.
Hata hivyo, ameeleza kuwa suala la afya, hasa uwezo wa kuona rangi kwa usahihi, ni jambo linalopewa kipaumbele kikubwa kwa wanaotaka kuwa marubani.
Chuo cha NIT kimekuwa mstari wa mbele katika kuendeleza rasilimali watu katika sekta ya usafirishaji, na kuanzishwa kwa kozi ya urubani ni hatua nyingine muhimu katika kujenga uwezo wa ndani wa wataalamu wa anga nchini.