Na Lucy Ngowi
ARUSHA: WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, ameongoza uzinduzi rasmi wa Programu ya Samia Extended Scholarship uliofanyika katika Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela (NM-AIST), jijini Arusha.

Katika uzinduzi huo, Mkenda amesema serikali imejizatiti kuwekeza kwa dhati katika vipaji na maarifa ya vijana, bila kujali hali ya kifamilia.
Amesema mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2024/2025, na kwamba unalenga kuleta usawa wa fursa kwa vijana wenye uwezo mkubwa wa kitaaluma, hasa katika sayansi na teknolojia.
“Kwa mara ya kwanza, haijalishi uwezo wa familia yako bali uwezo wa kichwa chako. Ukiteuliwa, usiombe chuo kingine. Njoo NM-AIST uandaliwe kwa miezi 10 utapewa laptop, utasoma kozi za awali, na kujiandaa kwa maisha ya kitaifa na kimataifa.” amesema.

Waziri huyo amesema katika awamu ya kwanza ya utekelezaji, wanafunzi 700 watapata ufadhili kamili, kati yao 50 bora zaidi wataenda kusoma katika vyuo vikuu vinavyoongoza duniani kama vile Massachusetts Institute of Technology (MIT) – Marekani, University of Oxford – Uingereza, Indian Institute of Technology Madras (IIT Madras) – India na Peking University – China,
Huku wengine 650 wakisoma ndani ya nchi katika taasisi zilizoteuliwa.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dkt. Amos Nungu amesema programu hiyo si mpango wa kawaida wa ufadhili wa masomo, bali ni sehemu ya mkakati mpana wa taifa wa maandalizi ya kushiriki kikamilifu katika Mapinduzi ya Nne ya Viwanda.
“Huu ni uwekezaji wa kitaifa na wa kizalendo. Tanzania haiwezi kubaki nyuma katika Mapinduzi ya Nne ya Viwanda,” amesema Dkt. Nungu, akiweka bayana umuhimu wa kuwekeza kwenye teknolojia na maarifa kwa vizazi vijavyo.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa NM-AIST, Profesa Nicholaus Kipanyula, amesema chuo hicho kinajivunia kuaminiwa na serikali kuendesha programu hiyo na kuwa sehemu ya maandalizi ya wataalamu mahiri wa teknolojia kutoka Tanzania.
“Kupitia programu hii, NM-AIST inakuwa kiini cha mapinduzi ya elimu ya kisasa nchini. Tunashukuru Wizara na Serikali kwa kutuamini,” amesema.
Programu ya Samia Extended Scholarship inatekelezwa kwa ushirikiano kati ya NM-AIST, COSTECH, Wizara ya Elimu, wataalamu wa Kitanzania waliopo nje ya nchi (diaspora), pamoja na taasisi za kimataifa.
Lengo kuu ni kuinua Tanzania kuwa miongoni mwa mataifa yanayoongoza kwa maarifa na ubunifu wa kiteknolojia.
Kwa mujibu wa Wizara ya Elimu, programu hiyo inalenga kuhakikisha vijana wenye vipaji hawazuiliwi na changamoto za kiuchumi, bali wanapewa fursa ya kuchangia maendeleo ya taifa kupitia taaluma zao.