Na Lucy Lyatuu
SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limeibuka mshindi katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, maarufu kama Sabasaba, baada ya kutuzwa kwa mchango wake mkubwa katika kulinda mazingira kupitia matumizi ya nishati safi.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa TPDC, Maria Mselemu, amesema hayo mara baada ya kupokea Tuzo na kuongeza kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya utendaji kazi wa hali ya juu na ufuatiliaji makini wa shughuli za shirika hilo.
“Hii ni tuzo yetu ya tano katika maonesho haya, na kwetu sisi imekuwa kawaida kupata tuzo kutokana na ubora wa huduma na miradi yetu, ikiwemo tuzo ya mazingira tuliyopokea leo,” amesema Bi. Mselemu.
Amefafanua kuwa TPDC imefanikiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa utoaji wa hewa ukaa kwa kutumia nishati safi ya kupikia na ile inayotumika katika magari, hatua ambayo imechochea mafanikio yao katika nyanja za mazingira.
“Kupitia matumizi ya nishati safi, tumeweza kuondoa zaidi ya tani 100,000 za hewa ukaa. Hii ni hatua kubwa katika kulinda mazingira yetu. Tunajivunia kuwa sehemu ya suluhisho la mabadiliko ya tabianchi,” ameongeza Mselemu.
.