Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umewataka Watanzania kubadili mtazamo hasi kuhusu gharama ya matumizi ya nishati safi ya kupikia, ukisisitiza kuwa kwa maendeleo ya sasa ya kiteknolojia, matumizi ya nishati hizo si tu yanapunguza gharama za muda mrefu, bali pia yanaboresha afya na kulinda mazingira.
Akizungumza katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba), katika Banda la REA, Mkurugenzi wa Umeme Vijijini, Jones Olotu amesema dhana kuwa nishati safi ni ghali ni potofu na haina msingi wa kitaalamu.

“Kumekuwepo na dhana kwamba kutumia nishati safi ya kupikia, ikiwemo umeme, ni gharama kubwa ukilinganisha na kuni au mkaa.
“Ukweli ni kuwa sasa teknolojia imeboreshwa sana. Majiko haya ni rafiki kwa mtumiaji, yanapunguza muda wa kupika na gharama za muda mrefu za manunuzi ya kuni na mkaa,” amesema.
Katika kutekeleza agizo la Rais wa Samia Suluhu Hassan, REA imeanza kuhamasisha taasisi zinazolisha zaidi ya watu 100 kutumia nishati safi ya kupikia.

Hadi sasa, maeneo 211 ya Jeshi la Magereza, yakiwemo magereza, kambi, shule, vyuo na hospitali yameanza kutumia nishati safi kwa mfumo wa bayogesi, LPG, gesi asilia na mkaa mbadala.
Aidha, maofisa zaidi ya 280 wa Jeshi la Magereza wamejengewa uwezo kuhusu matumizi sahihi na endelevu ya nishati safi ya kupikia ili kuhakikisha mabadiliko haya yanafanikiwa kwa uendelevu.
REA inasisitiza kuwa mapinduzi ya matumizi ya nishati safi si suala la kifahari bali ni hitaji la msingi kwa maendeleo ya taifa, afya ya wananchi, na uhifadhi wa mazingira. Watanzania wote wanahimizwa kutembelea Banda la REA katika Maonesho ya Sabasaba kujionea teknolojia hizi na kujifunza kwa vitendo njia mbadala, salama na nafuu za kupikia.
–