Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: Bodi ya Wataalam wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) imetangaza kuendesha mitihani yake ya 31 ya kitaaluma kuanzia Agosti 25 hadi 29, 2025 katika jiji la Dodoma.
Akizungumza na vyombo vya habari, Mkurugenzi Mtendaji wa PSPTB, Godfred Mbanyi, amewataka waombaji wote wenye sifa na nia ya kufanya mitihani hiyo kuhakikisha wanajisajili kwa wakati kupitia tovuti rasmi ya usajili https://registration.pstpb.go.tz.
Mbanyi amesema Agosti 15, 2025 ni tarehe ya mwisho ya usajili na amesisitiza kuwa mitihani hiyo itafanyika katika kituo kimoja tu, jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mbanyi amewaomba wazazi na walezi kuunga mkono ndoto za watoto wao kwa kuwalipia ada ya usajili wa mitihani hii muhimu, akisema kuwa elimu ya kitaaluma ni msingi wa maendeleo ya mtu binafsi na Taifa kwa ujumla.
Aidha, amewahimiza wadau wote wa sekta ya ununuzi na ugavi kufanya kazi kwa uadilifu na uzalendo, akisisitiza kuwa taaluma hiyo ni mhimili muhimu katika kuhakikisha matumizi bora ya rasilimali za umma kwa maslahi ya nchi.
Mitihani ya PSPTB ni sehemu muhimu ya mchakato wa kuthibitisha umahiri wa wataalamu wa ununuzi na ugavi, na hutoa nafasi kwa watahiniwa kupata ithibati ya taaluma hiyo kwa viwango vya kimataifa.
Amesema ili kupata taarifa zaidi kuhusu mitihani na usajili, wahusika wanahimizwa kutembelea tovuti rasmi ya PSPTB au kuwasiliana na ofisi zao zilizoko Dodoma.