Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: CHUO cha Ufundi Stadi (VETA), Kihonda mkoani Morogoro kimetengeneza mashine ya kusaga chumvi, kutoka kwenye mfumo wa mawe iwe kwenye chenga chenga ndogo ndogo.
Mkufunzi Mwandamizi wa Chuo hicho, Fredrick Uliki amesema hayo alipozungumza na Mfanyakazi Tanzania kuhusu changamoto inayowakabili wakulima wa chumvi, katika maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara yajulikanayo kama Sabasaba yanayoendelea mkoani Dar es Salaam.
Urick amesema chuo hicho kimetengeneza mashine hiyo baada ya kubaini changamoto iliyokuwa ikiwakabili walimaji wa chumvi katika eneo la Bagamoyo Pwani na Lindi.
“Wanafunzi wetu walifika maeneo hayo wakakuta wakulima wengi wa chumvi hawana kifaa cha kuwarahisishia kusaga chumvi kutoka kwenye mfumo wa mawe iwe kwenye mfumo wa chenga ndogo ndogo ambazo tayari kwa ajili ya matumizi baada ya kuweka dawa ile ya madini joto.
“Kwa hiyo wanafunzi walivyofanya tafiti zao wakaja na mashine hii, na mashine hii sasa baada ya kuona kuna fursa sasa ya kibiashara ya kimataifa hapa tutapata watu wengi watakaohitaji huduma yetu,” amesema.
Amesema inawezekana maeneo mengine pia wana shida ya kusaga chumvi kama ilivyo hayo maeneo mawili, wakaweza kupanua wigo wa huo ubunifu na kuingiza kwenye biashara ili chuo kipate mapato ya kurejesha malighafi ambazo zimetengenezea mashine hiyo.
“Wajasiriamali wa chumvi wakisaga chumvi yao kwa kutumia mashine hii itawaongezea thamani, wataweza kufungasha katika ukubwa wowote na kuuza kwa bei ya juu zaidi, na ikakaa kwa namna ya usafi.
“Tunawakaribisha wajasiriamali hao wafike kwenye banda la VETA, wajionee walete familia zao waweze kusoma VETA,” amesema.