Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: UTAFITI wa kutumia akili mnemba kwenye masuala ya magonjwa unaofanywa na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), utawarahisishia watafiti kupata majawabu mbalimbali ya magonjwa yanayotokea katika jamii.
Mfanyakazi Tanzania imefika katika Banda la UDOM kwenye maonesho ya Sabasaba kwa mwaka huu 2025, na kujionea jinsi tafiti inayoitwa conizuroai.com inavyowezesha upatikanaji wa majawabu ya kugundua dawa.
Mtafiti kutoka UDOM, Jospeter Jonathan amesema nchini Tanzania kuna changamoto ya kukosekana kwa njia mbadala na wataalam wa kuifanya njia hiyo kuwa nyepesi ya kupata tiba ya dawa kwa ajili ya magonjwa tofauti.
“Baada ya kuona changamoto hiyo, tumefanya utafiti kupitia tafiti inayoitwa conizuroai.com itakayokuwa inamsaidia mtafiti ambaye anajihusisha na ugunduzi wa dawa kufanya process kwa njia rahisi na kwa njia nyepesi ikilinganishwa na njia zilizokuwepo ambazo zinahitaji muda mwingi sana, gharama na zinahitaji ujuzi mkubwa.
“Kwenye eneo la ujuzi, kuna wataalamu wengi nchini lakini wameweza kukosa njia zinazoweza kuwasaidia kwenye tafiti zao kama hiyo,” amesema.
Ameongeza kuwa utafiti huo unatumia akili mnemba kwa ajili ya kuwasaidia hao watafiti ugunduzi wa tiba ya magonjwa tofauti tofauti ambayo watapenda kudadisi na kuweza kuleta tiba yake.
“Kwa sasa inatumika na watafiti tofauti katika Chuo Kikuu cha Dodoma na kupitia nafasi ya kufika Sabasaba tunaendelea kupata watafiti mbalimbali wa taasisi mbalimbali ambao wanaupenda huo mfumo na wameanza kuutumia,” amesema.
Amesema mategemeo yao ndani ya mwaka mmoja au miwili watapata watafiti wengi ambao watapeleka mapendekezo ya tiba ya magonjwa tofauti na kuweza kuchagiza tiba mbadala za magonjwa hayo kwa njia rahisi na nyepesi.