Na Daonso Kaijage
DODOMA: SERIKALI kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), imezindua rasmi mitambo 10 ya uchorongaji kwa ajili ya wachimbaji wadogo yenye thamani ya Sh. Bilioni 12.41.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema serikali imedhamiria kuwawezesha wachimbaji wadogo ili wainuke kiuchumi na kuchangia kikamilifu katika ukuaji wa pato la taifa pamoja na kukuza vipato vyao binafsi.
“Serikali inatambua mchango mkubwa wa wachimbaji wadogo katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii ndiyo maana Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025 imeelekeza kuwasaidia kwa kuwatengea maeneo,

“Kuwawezesha kufanya utafiti, kuwapatia mitambo ya uchorongaji na uchimbaji wa madini kwa njia za kisasa,” amesema.
Majaliwa amesema mitambo hiyo iliyonunuliwa ni mwendelezo wa juhudi zilizowekwa na serikali, ambapo Rais Samia alizindua mitambo mitano Oktoba 2023 ambayo tayari imeanza kutumika na kutoa mchango mkubwa kwa wachimbaji.

Amesema kupitia mitambo hiyo, wachimbaji wadogo wameanza kuaminiwa na taasisi za kifedha, hivyo kuongeza uwezo wao wa kukopesheka.
Wqziri Mkuu Majaliwa amesema mitambo miwili kati ya hiyo 10 imetengwa mahususi kwa ajili ya kuwahudumia wanawake wachimbaji, ikiwa ni sehemu ya kujumuisha jinsia zote katika fursa za kiuchumi kupitia sekta ya madini.

Katika tukio hilo, STAMICO limesaini mkataba rasmi wa ushirikiano na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), ili kuhakikisha watumiaji wa mitambo hiyo ya kisasa wanajifunza matumizi sahihi na ya kitaalamu ili kuendesha mitambo hiyo.
Majaliwa amepongeza juhudi za STAMICO na kuwataka wachimbaji kuhakikisha wanauza madini yao katika viwanda vya kusafisha dhahabu na kwenye masoko rasmi ili kukomesha biashara haramu na utoroshaji wa madini.
Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha usimamizi wa masoko 43 ya madini na vituo 109 vya ununuzi, ili kuleta mazingira bora ya kibiashara na kuhakikisha wachimbaji wadogo wanapata masoko yenye uhakika.
Mitambo 10 Ya Uchimbaji Madini Yenye Thamani Ya Bilioni 10 Yazinduliwa
Kwa upande wake, Waziri wa Madini Anthony Mavunde ameeleza kuwa tukio hilo ni ushuhuda wa namna Shirika hilo lilivyopiga hatua katika miaka ya karibu, na kuanza kujitegemea sambamba na kutoa gawio Serikalini.
“Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo na usimamizi wake wa Sekta ya Madini ambao leo umetufikisha hapa, mbali ya kununua mitambo hii, STAMICO pia inajenga kiwanda kikubwa cha kuchakata Madini ya Chumvi Wilayani Kilwa Mkoa wa Lindi,
“Hatua itakayowasaidia wakulima wa chumvi kupata soko la uhakika na bei nzuri,” amesema Mavunde.
Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt.Venance Mwasse amesema uzinduzi wa mitambo hiyo na vitendea kazi ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa Serikali kuhakikisha Shirika hilo linafanya shughuli zake kwa tija zaidi.
“Waziri Mkuu, Mitambo hii ya uchorongaji uliyozindua leo, ina faida nyingi kwa wachimbaji wadogo, hasa ikizingatiwa kuwa teknolojia hii inaleta mabadiliko makubwa katika utafutaji na uchimbaji wa madini kwa ufanisi na usalama zaidi.
“Ikiwemo kuboresha Utafiti wa Madini ambapo huwasaidia wachimbaji wadogo kuchimba kwa kina na kupata taarifa sahihi kuhusu tabaka la ardhi na uwepo wa madini kabla ya kuanza kuchimba kiholela.
“Hii huongeza nafasi ya kugundua mashapo ya madini yenye tija,” amesema.