Na Danson Kaijage
DODOMA: KUONGEZEKA kwa shughuli za kilimo nchini, kunasababisha uwepo wa visumbufu vya mazao wakiwemo kwelea kwelea kwa kuwa kunachangia kupungua au kutoweka kwa chakula halisi cha ndege hao.
Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Kanda ya Kati Dkt. Secilia Mroso amesema hayo alipozungumza na Mfanyakazi TANZANIA kwenye banda la maonesho katika Wiki ya Utumisihi wa Umma, kwenye viwanja vya Chinangali Jijini Dodoma.
Amesema kutokana na changamoto hiyo ya visumbufu vya mazao, mamlaka hiyo imenunua ndege mpya ya kisasa aina ya Thrush 510P2+ kwa ajili ya udhibiti wa viuatilifu hivyo.
Pia amesema mabadiliko ya tabia nchi yamechochea kuwepo kwa visumbufu vya mimea, na kutokea kwa makundi makubwa ya visumbufu vya mimea ambavyo kwa sasa vinadhibitiwa kwa urahisi zaidi kutokana na uwepo wa ndege hiyo.
Amesema TPHPA inaendelea kutoa elimu kwa wakulima namna ya kulima mazao yanayoendana na hali ya hewa pamoja na utumiaji mbegu bora na za kisasa zinazoendana na hali halisi ya eneo.
Amesema kwa sasa mamlaka hiyo itatekeleza shughuli zake za udhibiti wa visumbufu vya mazao kwa urahisi baada ya kununua ndege hiyo.
Amesema kabla ya kununua ndege hiyo, Mamlaka hiyo ilikuwa ikitumia ndege kutoka nchini Kenya na wakati mwingine ilichelewa kutokana na kuhudumia maeneo mengine yaliyovamiwa na visumbufu vya mazao.