Na Danson Kaijage.
DODOMA: JUMLA ya Mikoa 25 imefikiwa na Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, toka kuzinduliwa kwake Aprili mwaka juzi 2023.
Waziri wa 0katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro amesema hayo alipotoa taarifa kwa Waandishi wa Habari juu ya mafanikio ya Wizara hiyo kwa kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Amesema Ili kuhitimisha nchi nzima kwa upande wa Tanzania Bara, katika Mkoa wa Dar es Salaam kampeni hiyo itatekelezwa Juni, 2025.
Amesema upande wa Tanzania Zanzibar, utekelezaji wa Kampeni hiyo umefanyika katika mikoa mitatu na hivyo kukamilisha maeneo yote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania isipokuwa Dar es Salaam.

Amesema Kupitia Kampeni hiyo, jumla ya Halmashauri 180, Kata 1,907 na Vijiji/Mitaa 5,702 ilifikiw, na jumla ya wananchi 2,698,908 walifikiwa na kupata elimu na huduma za kisheria kupitia mikutano ya ana kwa ana.
Pia amesema Idadi ya Mashirika yanayotoa Huduma za Msaada wa Kisheria yameongezeka kutoka 84 Novemba, 2021 hadi 377 mwaka 2025.
Vile vile idadi ya Wasaidizi wa Msaada wa kisheria imeongezeka kutoka 617 mwaka 2021 hadi 2,205 mwaka 2025.
Katika hatua nyingine amesema Serikali imeanzisha madawati ya Msaada wa Kisheria katika Mamlaka za Serikali za Mitaa 184.

Na jumla ya watumishi 449 wameajiriwa ili kuwezesha nadawati hayo kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
“Tangu kuanzishwa kwa madawati hayo, jumla ya wananchi 6,427,738 wamepatiwa elimu juu ya masuala ya kisheria na haki za binadamu.
“Wizara kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imekamilisha uhakiki wa mwisho wa Sheria Kuu 300 kati ya 446 zilizotafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili.
“Hii ni sehemu ya jitahada za Serikali katika kuimarisha utawala bora, utawala wa sheria na kuimarisha misingi ya utoaji haki.
“Serikali imeanzisha Kituo cha Huduma kwa Mteja ambapo mwananchi hupata fursa ya kuwasilisha malalamiko na hoja mbalimbali za kisheria moja kwa moja,” amesema.