Na Danson Kaijage
DODOMA: WIZARA ya Madini imejipanga kununua chopa ambayo itafungwa mitambo kwa ajili ya kufanya utafiti wa kina nchi nzima kwa lengo la kubaini kiwango cha madini yanayopatikana na aina yake.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Madini Anthony Mavunde alipokuwa akitoa taarifa ya maendeleo ya Wizara hiyo kwa Waandishi wa Habari wa vyombo mbalimbali kwa kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan katika Ukumbi wa Idara ya Habari-Maelezo Jijini Dodoma.

Mavunde amesema chopa itakayonunuliwa na kufungwa mitambo ya kufanya utafiti wa madini nchini itakuwa na uwezo wa kubaini kitu kilichopo chini ya ardhi kwa umbali wa mita 500.
Amesema kwa nchi ya Tanzania licha ya kuwa inafanya vizuri katika sekta ya madini lakini bado, kwani ni asilimia 16 tu ya utafiti uliofanywa ambao unakubalika kimataifa.
“Tutakapokuwa na chopa ambayo itafungwa mitambo ya kisasa ya kufanya utafiti wa kubaini madini na aina yake tutaweza kufanya utafiti wa kina ambao unakubalika kimataifa.

“Kwa kutambua umuhimu wa sekta ya madini Rais Samia ameipatia sekta hiyo pesa nyingi,kwa mwaka wa fedha 2024/25 tulipatiwa bajeti ya Sh. Bilioni 231 kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yake na pesa nyingi imewekezwa kwenye utafiti.
“Kwa sasa utafiti kina uliofanywa nchi nzima ni asilimia 16 tu lakini mkakati uliopo ni ifikapo 2030 kutakuwepo na asilinia 50 ya upimaji wa kina nchi nzima na hapa sekta ya madini itakuwa na uhakika wa kutambua kiasi cha madini yanayopatikana nchini na aina zake,” amesema.
Amesema jambo lingine la mafanikio ni ujenzi wa maabara kubwa na ya kisasa itakayojengwa Dodoma eneo la kizota jambo ambalo ameeleza kuwa ni kuyaongezea madini thamani.
Hata hivyo ameeleza kuwa kwa sasa madini yanalenga kumnufaisha mtanzania mzawa yakiwemo makundi ya vijana,wanawake na makundi maalum.