Na Mwandishi Wetu
Morogoro: MFUKO wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umeendelea kudhihirisha mafanikio ya uwekezaji wake mkubwa katika sekta ya viwanda kupitia mradi wa kimkakati wa kiwanda cha sukari cha Mkulazi kilichoko mkoani Morogoro.
Kiwanda hicho kimeanza rasmi uzalisha Julai mwaka jana, 2024 kimezalisha ajira kwa watanzania na kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii.
Akizungumza wakati wa ziara ya Bodi ya Wadhamini ya NSSF, Mwenyekiti wa Bodi hiyo Mwamini Malemi ameeleza kuridhishwa na maendeleo ya mradi huo unaotekelezwa kwa ubia kati ya NSSF na Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Magereza.
“Nawapongeza kwa kazi nzuri, hongereni sana. Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini tumejionea na tunathamini mnachokifanya,” amesema hayo baada ya kupokea taarifa ya Kiwanda kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Kampuni Hodhi ya Mkulazi (MHCL), Selestine Some.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba amesema kupitia ziara hiyo ya kikazi, wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wameweza kushuhudia shughuli mbalimbali za uendeshaji wa mradi huo ulioanzishwa na Serikali kwa lengo la kupunguza nakisi ya sukari nchini.
Akisoma taarifa ya mradi, Mtendaji Mkuu wa Kampuni Hodhi ya Mkulazi Some amesema katika msimu wa mwaka 2024/25, kampuni ilipanga kuzalisha tani 20,000 za sukari ya majumbani, ambapo hadi mwisho wa msimu kiasi cha tani 19,124 sawa na asilimia 96 kimezalishwa.
Amesema katika msimu wa 2025/26 kampuni itaanza pia kuzalisha sukari ya viwandani ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa wakati wa uzinduzi wa kiwanda uliofanyika Agosti nane, 2024.
Some amesema uzalishaji wa sukari ya viwandani utapunguza uagizwaji wa bidhaa hiyo nje ya Nchi.
Amesema pia katika msimu wa uzalishaji wa sukari 2024/25 kiwanda kimetoa ajira za moja kwa moja kwa Watanzania 2,172 na zisizo za moja kwa moja 8,000, na kuongeza biashara, shughuli za kiuchumi na kipato kwa Wananchi wa Mji wa Dakawa, Dumila na vijiji jirani.