Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM:MASHINDANO ya Lugha na Tamaduni za Kichina kwa Wanafunzi wa Shule za Msingi yanapima kiwango chao cha uelewa ili wapangwe kwa kuzingatia ufaulu wao kuanzia mtu wa kwanza hadi wa nne.
Mwakilishi wa Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Flora Magige amesema hayo wakati akifungua mashindano hayo yaliyofanyika chuoni hapo ambayo yamewashirikisha wanafunzi 15 wa Shule za Msingi.
Profesa Magige amesema Mashindano hayo ni kipimo kizuri kwa mwalimu kujua uwezo wa mwanafunzi na kuona ni wapi aweke mkazo zaidi.
Pia amesema suala la ushiriki wa wanafunzi hao ni hatua muhimu kwa kuwa kila mmoja amejiamini na kushiriki mashindano hayo.
“Ninamtia moyo kila mmoja wenu hata Yule atakayeshika nafasi ya 15, kuna usemi unasema asiyekubali kushindwa sio mshindani, kwangu mimi wote ni washindi endeleeni kupambana bila kukata tama,” amesema.
Amesema amefurahi kusikia mashindano hayo ni watoto wa shule za msingi kwa kuwa inapendeza kuwaona wakishiriki kwa lengo la kujua lugha na tamaduni za kigeni ikiwa ni pamoja na kichina.
Naye Mkurugenzi Mtanzania wa Taasisi ya Kujifunza lugha ya Kichina ya Confucius, Dkt. Mussa Hans amesema katika mashindano hayo wanafunzi wameonyesha vipaji vyao vya kusimulia hadithi, kutoa hotuba, kughani mashairi ya kale na kuimba nyimbo mbalimbali wakitumia ishara mbalimbali na kuonesha hisia zao kuhusu kile wanachokiwasilisha.
“Kutokana na kuimarika kwa uhusiano wa kirafiki kati ya China na Tanzania, wadau wengi wamekuwa wakivutiwa kujifunza lugha na utamaduni wa kichina.
“Tunafurahi sana kuona kwamba wanafunzi wengi zaidi wa shule za msingi wanajifunza kichina katika umri mdogo.
“Tunaamini mbegu hizi zinazopandwa kwa wanafunzi hawa zitachanua na kuzaa matunda bora katika kujenga daraja la kuendelea kuimarisha urafiki kati ya China na Tanzania kwa sasa na baadaye,” amesema.
Amewaambia wanafunzi hao kuwa mashindano hayo yatakuwa ni kichocheo katika kuendelea kujifunza lugha na utamaduni wa kichina.
“Tunaamini kuwa katika kujifunza huku tutaendelea pia kujiimarisha katika kufanya kazi kwa bidii kuanzia katika umri wa utoto kwani hiyo pia ni sehemu ya utamaduni wa wachina,” amesema.
Naye Atka Said mwanafunzi wa darasa la nne katika Shule ya Nira Zanzibar amesema ameshiriki mashindano hayo kwa kuwa anapenda lugha hiyo.
Pia mwanafunzi Baraka Ramadhan wa Shule ya Msingi St. Mathew amesema ameshindana mashindano hayo kwa kuwa lugha hiyo ina utamaduni mzuri ikiwemo kuimba na kucheza.