Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: MWANAFUNZI wa mwaka wa nne Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Felechi Raymond ameongezea thamani zao la korosho na stafeli kwa kutengeneza mtindi.

Raymond amesema hayo alipozungumza na Mwandishi wa habari hizi katika Wiki ya Utafiti na Ubunifu kwa mwaka huu 2025, chuoni hapo.
Amesema,” Kwa nini nimeamua kutumia korosho na stafeli. Korosho inalimwa sana katika nchi ya Tanzania, lakini uchakataji wake ndani ya nchi ni mdogo.
” Kwa hiyo nataka kuongeza thamani ya zao la korosho lakini pia kutumia tunda la stafeli kwa sababu lina virutubisho vinavyozuia kupata saratani lakini pia kuna nyuzi nyuzi muhimu kwa ajili ya afya ya mfumo wa umeng’enyuaji wa chakula,”.
Amesena pia ameamua kuongezea thamani tunda la stafeli kwa kuliweka katika mtindi ili thamani yake iweze kupanda, iweze kukaa muda mrefu na kuwafikia wengi.

Amesema bidhaa hiyo ni nzuri na ina faida kuliko ile inayopatikana kwenye bidhaa ya wanyama .
” Inasaidia kushusha lehemu kwenye damu , zikishushwa inapunguza uwezekano wa kupata magonjwa ambayo yanahusiana na kuziba kwa mishipa ya damu na moyo,” amesema.
Pia amesema bidhaa hiyo ina nyuzi nyuzi zinazotokana na tunda la stafeli, ni muhimu katika afya ya utumbo au mfumo wa kumeng’enya chakula.
” Ukiachana na faida ya lishe kuna watu hawawezi kutumia maziwa au bidhaa zinazotokana na wanyama kwa sababu wana ‘aleji’ nazo au wakitumia wanapata shida hivyo bidhaa hiyo inawalenga watu hao pia.