Na Mwandishi Wetu
SERIKALI kupitia Ofisi ya Rais – TAMISEMI imesema itaendelea kukarabati hospitali zote Kongwe kupitia mpango mkakati wa ukarabati, na upanuzi wa hospitali kongwe za halmashauri ,vituo vya afya Pamoja na zahanati ili kuboresha miundombinu ya huduma za afya kote nchini.
Hayo yamesemwa leo Mei 07, 2025 bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri Ofisi ya Rais – TAMISEMI Dkt. Festo Dugange wakati akijibu swali la nyongeza la Shally Raymond, mbunge wa viti maalum mkoa wa Kilimanjaro kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais -TAMISEMI. Mohamed Mchengerwa.
Mbunge huyo, alitaka kujua ni lini serikali itaipa kipaumbele cha ukarabati wa miundombinu zahanati ya Rononi iliyoko Uru Kaskazini mkoani humo.
Katika majibu yake Naibu Waziri Dkt. Dugange amesema tayari serikali imeweka mpango mkakati wa ukarabati na upanuzi wa vituo vyote kongwe vya kutolea huduma za afya, ambapo tayari ukarabati na upanuzi umeanza katika ngazi ya hospitali Kongwe za Halmashauri, na baada ya hospitali za halmashauri, vitafuata vituo vya afya na zahanati zote Kongwe ambazo zinahitaji ukarabati.
Dkt. Dugange amewaelekeza wakurugenzi kwa halmashauri zenye vituo vya kutolea huduma za afya vinavyokabiliwa na uhaba wa vifaa pamoja na changamoto ndogondogo kama vile samani kutumia fedha za mapato ya ndani ili kumaliza changamoto hizo haraka iwezekanavyo