– Kukutanisha Watunga Sera, Wafanya Biashara, Watafiti, Wataalam Wa Kodi
Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM; CHUO cha Kodi (ITA), kimeandaa kongamano la kwanza la kodi litakalo wakutanisha watunga sera, wafanya biashara, watafiti na wataalam wa kodi kwa ajili ya kujadili mikakati ya kupanua wigo wa kodi na kuimarisha ulipaji kodi kwa hiari ili kuongeza mapato ya serikali.
Mkuu wa chuo hicho cha ITA, Profesa Isaya Jairo amesema hayo alipotoa taarifa kwa vyombo vya habari juu ya kongamano hilo litakalofanyika Dar es Salaam Mei nane, mwaka huu katika hoteli ya Rotana.
Amesema chuo hicho ambacho ni sehemu ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kimeandaa kongamano hilo lenye mada kuu isemayo , ” Kuongeza wigo wa kodi na kuimarisha ulipaji kodi kwa hiari Tanzania,”.
Amesema mada ambayo washiriki watajadili ili kupanua wigo wa kodi na kuimarisha sekta isiyo rasmi.
“Washiriki watajikita zaidi kujadili uimarishwaji wa ulipaji kodi kwa hiari na kuongeza wigo wa kodi, mtazamo wa sekta binafsi na wafanya biashara.
“Pia tutajadili mikakati ya urasimishaji na motisha kwa kulipa kodi kwa hiari,, Mada ndogo nyingine itakayojadiliwa ni ukwepaji wa kodi, wakijadili mada hii, washiriki watajikita zaidi katika mikakati ya utupwaji wa bidhaa hafifu kutoka nje ya nchi na kuongeza uhiari wa kulipa kodi,” amesema.
Amesema kongamano hilo linafanyika wakati TRA inafanya mageuzi mbalimbali katika kuongeza ulipaji wa kodi kwa hiari kwa kutumia teknolojia ya mawasiliano,
Kupambana na ukwepaji wa kodi na kurasimisha sekta isiyo rasmi.
” Hata hivyo jitihada hizo zinaathiriwa na sekta isiyo rasmi kuchangia kiasi kidogo cha asilimia 45 katika pato la taifa wakati ikiwa na kiasi kikubwa cha nguvu kazi lakini chenye kiwango kidogo cha ulipaji kodi kwa hiari,” amesema.
Amesema matrajio yao ni kwamba kongamano hilo litaangalia mikakati ya kupanua wigo wa kodi, kupata utambuzi wa tabia katika kuongeza ulipaji kodi kwa hiari,
Kuchunguza njia za kuboresha usawa wa kodi na kupunnguza taratibu zisizo rasmi, kuimarisha ushirikiano kati ya wadau , kuteggemea matumizi ya teknolojia katika usimamizi wa kodi na kutengeneza mapendekezo ya sera yanayotekelezeka.