Na Danson Kaijage
DODOMA: WATU wenye ulemavu wa ngozi Mkoani Dodoma wamepatiwa msaada wa vifaa mbalimbali vitakavyowasaidia kupambana na hali yao ya ulemavu.
Benki ya NMB imetoa vitu mbalimbali yakiwemo mafuta maalum kwa ajili ya kujikinga na mionzi ya jua inayosababisha saratani ya ngozi kwa watu hao.
Meneja wa NMB Kanda ya kati Janeth Shangwe, akikabidhi msaada huo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi inayojihusisha na masuala ya watu wenye ulemavu ya Foundation For Disabilities Hope (FDH), Maiko Salali amesema tukio hilo ni sehemu ya kutekeleza takwa na taasisi kuresha kwa jamii kile wanachokipata.
“Sisi kama NMB kutoa msaada kwa jamii imekuwa ni jambo letu na tumekuwa tukithamini watu wa aina mbalimbali,
“Tulipo pata maombi yenu kuwa mnahitaji vifaa kwa ajili ya kujingia na mionzi ya jua mara moja tuliona kuna umuhimu mkubwa kushirikiana na tutumie sehemu ya faida ambayo tunaipata kwa ajili ya kuleta msaada huu.
“Tunaamini kwa namna moja ama nyingine nyinyi kama Foundationa For Disabilities Hope hapa Dodoma mtaufikisha msaada huu kwa wengi ambao wanauhitaji na vitu hivi,” amesema.
Ametaja vifaa walivyotoa ni mafuta ya kujikinga na mionzi ya jua 200, kofia za jua 200 pamoja na miwani ya jua 200 vyote vikiwa na thamani ya Sh. milioni 20.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa FDH, Maiko Salali ameishukuru NMB, na kueleza jinsi benki hiyo inavyogusa makundi ya wenye ulemavu.
“Kupitia msaada huu mmerejesha matumaini kwa watu wenye ulemavu msaada huu kwetu sisi watu wenye ualibino mmetusaidia kuongeza kiwango cha kuishi sisi watu wenye ualibino tunakabiliwa na changamoto ya saratani ya ngozi, adui yetu namba moja ni jua,”amesema.
Amesema, mionzi ya jua inapowapiga kwenye ngozi wanatokwa na vidonda ambavyo badae vinakwenda kusababisha saratani ya ngozi.
“Hivyo hivi vifaa vya kujikinga na mionzi ya jua vinakwenda kuimarisha maisha yetu na kuweza kushiriki katika kulijenga taifa letu,” amesema.